Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imesema itaendelea kumshikilia Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Kigaila Benson.
Kigaila aliyeripoti Kituo Kikuu cha Polisi jana Jumatatu Oktoba 23,2017 na kuwekwa rumande, anatuhumiwa kutoa lugha za uchochezi Oktoba 12,2017 katika mkutano na waandishi wa habari.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 24,2017 mchana, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema, “Tunaendelea kumshikilia na kumhoji, tukimaliza yale ambayo yanamhusu tutampeleka mahakamani au kumpa dhamana na kama ushahidi utamhusu mtu mwingine atakayehitaji kutafutwa tutafanya hivyo. Tutakapomaliza tutarudi kwenu kuwaeleza hatua zaidi.”
Kamanda Mambosasa amesema Kigaila anatuhumiwa kutoa lugha zinazolenga kukashifu viongozi wa Serikali na Serikali yenyewe.
Awali, Mwanasheria wa Kigaila, Fredrick Kihwelo alisema anaendelea kufuatilia dhamana kwa kuwa makosa anayotuhumiwa kutenda mteja wake yana dhamana, hivyo hajui ni kwa nini hapatiwi haki hiyo.
Social Plugin