Mkuu wa shule ya Sekondari ya Mtenga wilayani Nkasi mkoani Rukwa Leonard Mwipugi (29) amejiua kwa kujikata kisu kwenye koromeo kutokana na wivu wa kimapenzi.
Akizungumzia tukio hilo mratibu wa elimu kata ya Mtenga Hebron Mwafungo ameiambia Malunde1 blog kuwa mwalimu huyo amekutwa akiwa amefariki dunia baada ya kujichinja nyumbani kwake Oktoba 20,2017 majira ya saa 6 mchana baada ya kutoka shuleni.
Alisema mwalimu siku ya tukio alikwenda kazini kwake shule ya sekondari Mtenga na majira ya 5 asubuhi alirejea nyumbani na hakumkuta mkewe nyumbani na baada ya muda walipata taarifa kuwa mwalimu huyo amekutwa amekufa baada ya kujichinja koromeo chumbani kwake
Alisema kuwa mwalimu huyo alikuwa akiishi na mdogo wake wa kike nyumbani hapo na alipofika nyumbani alimtuma mdogo wake huyo mbali na nyumbani kwake na baada ya kurudi aliona damu zimetapakaa sebuleni na baada ya kuchungulia chumbali alikuta kaka yake amefariki dunia kwa kujichinja ndipo alipotoa taarifa uongozi wa kijiji hicho.
Alisema baada ya kumhoji mdogo wa marehemu huyo alisema kuwa kaka yake siku za nyuma alikuwa na mgogoro na mkewe akimtuhumu kuwa si muaminifu katika ndoa yao lakini walizungumza na kuumaliza mgogoro huo.
Siku chache baadae mke wa marehemu huyo aliondoka nyumbani na kwenda mjini Namanyere bila kumuaga mume wake hivyo huenda jambo hilo lilimkasirisha kaka yake na kufikia uamuzi wa kujichinja.
Diwani wa kata ya Mtenga Pankrasi Maliyatabu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa baada ya tukio hilo walitoa taarifa polisi ambao walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya wilaya ya Nkasi.
Kamanda wa polisi mkoani Rukwa George Kyando alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa bado uchunguzi wa polisi unafanyika kufuatia tukio hilo.
Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Nkasi
Social Plugin