MTU na mkewe wameuawa kwa mapanga wakiwa wamelala nyumbani kwao kwa kinachodaiwa walikuwa na kesi mbili za kugombea ardhi Baraza la Ardhi la kata ya Hunyari, Tarafa ya Chamriho, Bunda, Mara.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Oktoba 22, mwaka huu, katika kijiji cha Mariwanda, Hunyari. Ofisa tarafa ya Chamriho, Boniphace Maiga jana alithibitisha na kuwataja waliouawa kuwa ni Magina Masengwa (61) na mkewe, Sumaye Sebojimu (58) wa kitongoji cha Kiborogota kijiji cha Mariwanda.
Maiga alisema wanafamilia hao walivamiwa usiku nyumbani kwao wamelala na kukatwa mapanga na watu wanaodaiwa walikuwa wameshitakiwa Baraza la Ardhi la Kata kuhusu kesi za migogoro ya ardhi.
Alisema baada ya kufanya mauaji hayo watuhumiwa walitoweka na kuziacha maiti za watu hao ndani ya nyumba hiyo na kesho yake asubuhi mjukuu wao aliyekuwa anakwenda shambani alifika nyumbani hapo kwa ajili ya kuwasalimia na ndipo alikuta wamekwishauawa na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
Alisema mtuhumiwa mmoja Nyangi Nyabirumo, mkazi wa kijiji hicho amekwishakamatwa na polisi.
IMEANDIKWA NA AHMED MAKONGO - habarileo BUNDA
Social Plugin