Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MVUA YALETA BALAA DAR,YAUA ..SABA WANUSURIKA.....ANGALIA PICHA HAPA

MVUA za vuli zilizoanza wiki zimesababisha madhara makubwa katika mikoa mbalimbali ikiwamo ya Pwani na Dar es Salaam kiasi cha barabara kufungwa, mabasi yaendayo haraka kusimamisha huduma kwa muda, watu wawili kufa na saba kunusurika kusombwa na maji.

Aidha, kwa mara ya kwanza Kituo cha kupimia mvua cha Kibaha mkoani Pwani kimetumia saa 24 kupima milimita 177.9 za mvua tangu kilipoanzishwa mwaka 1964, upimaji huo umeanzia juzi saa tatu asubuhi mpaka jana muda huo, hivyo kuweka rekodi.
Jijini Dar es Salaam, kutokana na mvua zilizonyesha katika maeneo mbalimbali kwa siku mbili mfululizo, Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimefunga kwa muda baadhi ya barabara ili kuzuia maafa zaidi yasitokee.
Kutokana na mvua hizo, vijana wawili wanadaiwa kupoteza maisha katika maeneo ya Tabata Kimanga na Mbezi Luis kutokana na kusombwa na mafuriko. Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Musilimu alitaja maeneo yaliyofungwa kwa muda kuwa ni Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani, Kibaha Mizani na Barabara ya Mwai Kibaki karibu na Daraja la Malecela.
“Barabara ya Morogoro kutoka Faya kwenda Magomeni imefungwa, pia barabara ya Jangwani Klabu ya Yanga kwenda Kigogo haipitiki na imefungwa...Pia nyumba za kando ya Bonde la Msimbazi zimefunikwa na maji,” alisema Kamanda Musilimu.
Alisema barabara nyingine zilizofungwa ni barabara ya Kawawa (Kigogo Sambusa), Kiluvya kwa Komba, Barabara ya Afrikana karibu na nyumbani kwa Jenerali mstaafu David Mwamunyange, ambako kuna daraja linalojengwa pamoja na barabara ya Bagamoyo eneo la Tegeta Nyaishozi mpaka Basihaya.
Aidha, kutokana na hilo, wananchi wanaotokea Morogoro kwenda Chalinze hadi Dar es Salaam, walishauriwa kutumia Barabara ya Bagamoyo, wanaotumia Barabara ya Mwai Kibaki watumie Barabara ya Coca-Cola kwenda Mwenge.
Aidha, Jeshi hilo lilielekeza askari wa kikosi hicho kwenda katika maeneo ambayo maji yanapita juu ya barabara ili kuzuia vyombo vya usafiri kutumia barabara hizo. Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema wamepata taarifa ya vifo viwili katika maeneo ya Tabata Kimanga na Mbezi Luis.
“Hadi sasa tuna taarifa ya vifo Tabata Kimanga katika Bonde la Mto Kenge ambapo kijana anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25-30 amepoteza maisha na hajatambuliwa na kijana mwingine ametumbukia na gari yake Mbezi Luis na hajatambuliwa,” alieleza Kamanda Mambosasa.
Alisema wanaendelea kufanya ufuatiliaji na tathmini zaidi ya maafa yaliyotokea kutokana na mvua hizo na watatoa taarifa kamili kwa wananchi. Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa kampuni ya inayotoa huduma kwenye mradi wa mabasi yaendayo haraka (UDART), Deus Bugaywa alisema huduma hiyo ililazimika kusitishwa kwa muda jana kutokana na kufungwa kwa Barabara ya Morogoro kwa sababu ya Daraja la Mto Msimbazi kujaa maji.
Hata hivyo, huduma ya mabasi yaendayo haraka iliendelea kutolewa kwa njia ya kutokea kituo cha Gerezani, Kariakoo kwenda Muhimbili. Kaimu Mkurugenzi Mkuu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya Hali ya Hewa wa Mamlaka ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Ladislaus Chang'a aliliambia gazeti hili kuwa mvua hizo kwa Kibaha ni za kiwango cha juu kurekodiwa tangu kituo hicho kilipoanzishwa.
“Tokea kituo hiki kilipoanzishwa, ndani ya saa 24 hatujawahi kupima mvua kubwa kiasi hicho. Mabadiliko ya tabianchi ulimwenguni viashiria vyake ni matukio ya mvua kubwa," alisema Dk Chang’a na kuongeza kuwa siku hiyo hiyo vipimo vilionesha kiwango cha mvua Pemba ilikuwa milimita 42.3, Zanzibar milimita 190.1 na Dar es Salaam milimita 153.3. Alisema katika utabiri wa kila siku unaotolewa na TMA, walitoa angalizo la uwezekano wa ongezeko la mvua maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.
“Hicho ndicho kilichotokea. Tunatarajia kuanzia leo (jana) mvua itaanza kupungua kidogo katika hayo maeneo,” alibainisha. Alisema ni vema jamii ikawa na tabia za kufuatilia taarifa ya hali ya hewa zinazotolewa na kuzingatia kupanga mipango ya kijamii na kiuchumi, kuweza kuongeza tija na ufanisi pia kuchukua tahadhari kubwa ya kuokoa mali na maisha.
Hivi karibuni, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alipotoa mwelekeo wa mvua za msimu, alisema mvua zinatarajia kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo mengi nchini.
Alisema matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanatarajiwa kusababisha mafuriko katika maeneo machache. Mkoani Pwani, watu saba wamenusurika kifo baada ya kusombwa na maji walipokuwa wakijaribu kuvuka huku wakiwa wameshikana mikono, ambao walijinusuru kwa kupanda kwenye miti kabla ya kuokolewa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Aidha, kati ya watu hao, mmoja alikuwa akining’inia kwa kujishika kwenye bomba la bango la matangazo huku mwili wake ukiwa ndani ya maji kwa zaidi ya saa huku akiwa anaomba msaada wa kuokolewa bila mafanikio.
Watu walionusurika ni Kenned Meshaki, Mohamed Kitindi, Mohamed Zimanya, Furaha Mwaipopo, Silas Moshi, Henry Francis na mwanamke mmoja ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja ambao wote walikimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Pwani ya Tumbi mjini Kibaha.
Tukio hilo lilitokea jana eneo la Maili Moja kwenye daraja linalotenganisha kati ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani na kusababisha daraja kujaa maji na kusababisha magari na watu kushindwa kuvuka upande wa pili.
Daraja hilo ambalo linapita kwenye Mto Mpiji lilikuwa halipitiki na kusababisha watu na abiria kushindwa kuvuka upande wa pili kutoka Maili Moja wilayani Kibaha na upande mwingine Kiluvya katika Wilaya ya Ubungo.
Kutokana na daraja hilo kushindwa kupitika, abiria wa mabasi walishindwa kuendelea na safari zao kupitia kwenye barabara ya Morogoro. Akizungumza na gazeti hili kwenye eneo la tukio hilo, Ofisa Habari na Uhusiano wa Jeshi la Uokoaji, Harrison Mkonyi alisema kazi ya uokoaji imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani wamewaokoa watu hao wakiwa salama.
“Tunawashukuru wadau mbalimbali vikiwemo vikosi vya majeshi ya Polisi, Magereza, JWTZ na wananchi ambao walionesha ushirikiano wa hali ya juu kuwanusuru watu hao akiwemo mwanamke mmoja,” alieleza.
Habari kwa hisani ya Habarileo




RPC Hamduni ameeleza kuwa taarifa za kijana huyo kuhusu majina yake bado hazija kamilika, na kuhusu uharibifu wa mali amehaidi kutoa ufafanuzi hapo baadae.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akimuonesha Mbunge wa jimbo la Ilala Mussa Hassan Zungu baadhi ya nyumba zilizoharibiwa na mvua (nyumba hazipo pichani)

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema amewataka wakazi wote wanaosihi maeneo hatarishi hususani Jangwani kuondoka mara moja kwani mvua hizi ni endelevu na huenda zikafika mpaka siku ya Jumamosi hivyo ni vyema kuchukua tahadhari kwa kuhama maeneo na kwenda maeneo yaliyo salama.


Mtandao huu ulitembelea eneo la Jangwani na kujionea miundombinu ilivoharibiwa na kupelekea suala la usafiri kuwa mtihani kwa wakazi wa maeneo mbali mbali ikiwemo Kimara, Mbezi nakadhalika, huku nyumba nyingi kwa asilimia kubwa zikiwa zimejaa maji. 


Barabara kuelekea Jangwani ikiwa imefungwa


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com