Mwalimu wa madrasa, Abdillah Sharifu, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kumlawiti mtoto wa kiume wa miaka 11.
Mshtakiwa anadaiwa kumlawiti mtoto huyo na pia kumtishia kuwa angemroga endapo angetoa taarifa kwa wazazi wake kuwa anamfanyia kitendo hicho.
Akisoma hukumu, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan amesema ameridhishwa na ushahidi wa mashahidi wanne akiwemo daktari.
“Mshtakiwa nimekutia hatiani kama ulivyoshtakiwa, ninakuhukumu kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwako na watu wengine wenye tabia mbaya kama hii,” amesema.
Hakimu Hassan amesema kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ambaye ni mwalimu wa dini ni cha kikatili.
Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa mshtakiwa alimfanyia ukatili huo, huku akimtishia kuwa iwapo angethubutu kutoa siri hiyo angemroga.
“Mara kwa mara alikuwa akinifanyia mchezo huu hadi nilipomwambia mama na kisha kwenda kufungua kesi katika kituo cha polisi Mazizini,” alisema mtoto huyo katika ushahidi alioutoa mahakamani.
Katika ushahidi wa mama mzazi wa mtoto huyo, alidai baada ya kuripoti polisi walikwenda hospitali ambako kwa mujibu wa vipimo vya daktari licha ya kutokuwa na michubuko ilionekana aliingiliwa.
Mshtakiwa alidai ana mke kipofu na kwamba, hafanyi vitendo hivyo isipokuwa alikuwa na ugomvi na mama wa mtoto huyo na ndiyo sababu ya kumfungulia kesi.
Hata hivyo, mshtakiwa alishindwa kuifafanulia Mahakama chanzo cha ugomvi hivyo ilitupilia mbali utetezi wake na kumtia hatiani.
Mshtakiwa alitenda kosa hilo, Februari 25 katika eneo la Moshi Bar, Gongo la Mboto.