PAROKIA MPYA YAZINDULIWA JIMBO KUU KATOLIKI DODOMA

KATIKA safari ya kueneza Injili kwa watu wote hapa duniani, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma limepata Parokia mpya ya Pwaga iliyozinduliwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo Mhashamu Beatus Kinyaiya OFM-Capp.


Akizindua parokia hiyo mpya hivi karibuni, Askofu Mkuu Kinyaiya OFM-Capp amesema kuwa safari ya injili ni ngumu na kuwa si vyema wanadamu kuipuuzia kwani ni safari ya toba huku Kanisa likiwa ni moyo wa muamini popote pale na kuwa pamoja na kuwa parokia hiyo mpya haina jengo kubwa lakini Kanisa ni watu na ni popote pale bila kujali ni wapi wanasalia, la msingi ni kuwa na imani kwa Mungu.


“Mama Kanisa anasisitiza watu kusali kwa moyo na nguvu kubwa bila kujali sala inafanyika wapi, mkristo anatakiwa kusalia mahali popote kwani sala ni Baraka na muamini anapata nafasi ya kuongea na Mungu na si Kanisa. Parokia ya Pwaga kwa uchanga wake wa majengo isiwe sababu ya kuibeza bali na itiwe nguvu na waamini wake kwa kusali kwa nguvu na kuwa suala la majengo makubwa na mazuri yatakuja baadaye.” Amesema Askofu Kinyaiya.

Amesema parokia mpya ya Pwaga imefunguliwa kutokana na mahitaji ya waamini kutaka huduma za kiroho kufanyika karibu nao na kuwa ombi hilo lilitolewa kwa marehemu Askofu wa pili wa Jimbo Kuu Dodoma Mhashamu Joseph Isuja Shungu miaka 30 iliyopita yaani mwaka 1987.

“Kristo hapatikani katika majengo mazuri bali anapatikana katika mioyo yenu, saline kwa nguvu msitafute pa kusalia bali pa kusalia pawe popote ili mradi mnasali kwa moyo na Kristo atapatikana hapo hapo mlipo, msifadhaike mioyoni mwenu. Majengo mazuri na makubwa yatakuja, ruhusuni Roho Mtakatifu aingie mioyoni mwenu atawaelekeza cha kufanya huku mkijitoa kama mlivyojitoa katika ujenzi wa nyumba hii ya mapadri.” Amesisitiza.

Amesema kwa sababu parokia hiyo ya Pwaga inaanza chini yake, ni vyema iwe kioo kwa ajili ya kufundisha watu kumuongokea Mungu huku akiwaonya wana kipaimara 26 aliowapa sakramenti siku hiyo kulisikia neno hilo na kulifuata.

Pamoja na kutangazwa kwa parokia hiyo mpya Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya OFM-Capp amemtangaza Padri Nestory Ngunwa kuwa paroko wa parokia hiyo mpya na kuwa kwa sasa atakuwa akikaa parokiani Lumuma hadi hapo nyumba mpya ya mapadri hapo Pwaga itakapomalizika.

Paroko wa Parokia hiyo mpya, padri Ngunwa amesema kuwa anamshukuru Mungu kwa kumuona, na kwa kutumwa na Askofu katika parokia hiyo, ataifanya kazi ya Bwana kwa moyo wote.


Parokia hiyo mpya ya Pwaga ina vigango 12 ambavyo ni Godegode, Mgoma, Kisisi, Tambukareli, Wisuzaje, Idibulilo, Lufu, Kidenge, Gomhungile, Munguwi, Idaho na Maswala .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post