Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amewapongeza viongozi waliohusika kuvunja nyumba ya CCM iliyokuwa imejengwa katika hifadhi ya barabara jijini Mwanza.
Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo alipokuwa akizindua daraja la kisasa la waenda kwa miguu la Furahisha jijini humo.
“Ile nyumba moja ya CCM nayo ilikuwa kwenye road reserve (hifadhi ya barabara). Nawashukuru viongzi wa mkoa kwa kulibomoa. Maendeleo yana madhara yake. Kwahiyo, nawashukuru Mkuu wa Mkoa, mmefanya vizuri sana,” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha wakazi wa jiji hilo kuwa alipokuwa Waziri wa Ujenzi alivunja ukuta wa nyumba yake iliyoko katika eneo la Selman Nasoro, tukio ambalo liliripotiwa na vyombo vya habari.
Amewataka wakaazi wa jiji hilo kukubali kupisha maeneo ya hifadhi ya barabara kwa ajili ya miradi inayolifaidisha taifa kama ilivyokuwa kwa mradi wa daraja la Furahisha.
Rais Magufuli amesema kuwa daraja hilo ambalo limejengwa vizuri limesaidia kuokoa maisha ya waenda kwa miguu ambao walikuwa wanagongwa na magari walipokuwa wakienda katika matamasha na mikutano mbalimbali katika viwanja vya Furahisha.
Alisema kuwa pamoja na kuondoa tatizo la foleni katika eneo hilo, daraja hilo linaweza kutumika kama kivutio cha utalii wa ndani kwani ni kioo cha jiji hilo.
Daraja hilo la Furahisha limegharimu zaidi ya shilingi bilioni nne.
Social Plugin