RAIS John Magufuli amesema atashangaa sana kuona fedha alizoidhinisha kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, hazitawafikia walengwa kwa wakati.
Katika hatua nyingine Rais, Magufuli ameagiza kufanyika kwa mabadiliko ya haraka katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili wizara hiyo iweze kujiendesha kwa kuzingatia diploma ya uchumi, kama chachu ya utekelezaji wa sera ya viwanda.
Alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana mara baada ya kuwaapisha Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Mabalozi, aliowateua juzi, tukio lililoambatana na viongozi hao kula kiapo cha maadili.
Rais Magufuli alisema mwezi uliopita Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa Sh bilioni 147 zilizoidhinisha kwenda Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu wanaostahili kupata.
“Nitashangaa sana kama patakuwepo wanafunzi waliopo kwenye orodha ya kupata mikopo na wawe hawajapata, nitashangaa sana kwa sababu mimi najua nimeshaidhinisha fedha hizo na zimeshatoka,” alisema Rais Magufuli.
Alisema anayasema hayo kwa sababu inaweza kutokea wanafunzi wakafungua vyuo na kuanza kuhangaika vyuoni bila kupata mikopo, jambo ambalo alisema hataki kulisikia. “Ndiyo maana wakati mwingine nalazimika kuwaza kuwa fedha zimewekwa benki kwenye fixed deposit (akaunti ya muda maalumu) zinamzalishia mtu,” alisema.
Aliwataka pia viongozi hao walioapishwa, kuzingatia sheria katika utekelezaji wa majukumu yao na pia wakawe watumishi wa watu hasa watu wanyonge. “Ninyi ni wawakilishi wa Watanzania, mkawe sauti na wasemaji wao, mkamtangulize Mungu katika kuwahudumia, mkizingatia hayo mtaweza kujibu hoja za Watanzania,” alisema Rais Magufuli.
Aliwataka viongozi katika ngazi zote, kuangalia vitu ambavyo wanaweza kufanya kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa wananchi wao. Aidha, Rais Magufuli alisema ameamua kufanya mabadiliko katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuleta matokeo ya haraka, kuendana na Tanzania ya Viwanda.
Alisema ili kuifanya wizara hiyo kuendana na diplomasia ya kisasa inayoegemea katika uchumi, ndiyo maana ameamua kumteua Profesa Adolf Mkenda ambaye ni mchumi kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo ili kuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi.
Kabla Profesa Mkenda alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Alisema anataka kuona kila balozi katika nchi anayowakilisha, anakuwa sehemu ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania na kwamba kuanzia sasa kila baada ya muda fulani, kila balozi ataeleza ameiletea nchi uwekezaji gani.
Alitaka pia kuwepo kwa mfumo maalumu wa kuwachagua watumishi wa serikali wenye uwezo kufanya kazi katika wizara hiyo, kwa vile hivi sasa kuna tabia watumishi wasiofaa serikalini, ndiyo wanapelekwa katika wizara hiyo kupumzika na wengine kupelekwa katika balozi mbalimbali wakiwa hawana uwezo.
Alisema balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali, zina watumishi wengi kuliko uhitaji, tofauti na balozi za nje nchini ambazo zina watumishi wa nchi hizo wachache na wanaajiri Watanzania kutekeleza majukumu mengine na kuleta ufanisi. Alimtaka Profesa Mkenda kuangalia dhana hizo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambaye sasa amemteua kuwa Mkuu wa Mkoa, Christina Mndeme atakuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na kubadilishana na Mkuu wa Mkoa huo, Dk Bilinith Mahenge ambaye sasa atahamia Dodoma.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewaagiza Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu kufika katika Studio za Televisheni ya Taifa (TBC), kueleza mafanikio ya serikali kama ilivyopangwa.
“Mawaziri, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu, TBC imetayarisha vipindi maalumu vya kuelezea mafanikio tuliyoyafikia katika miaka hii miwili, lakini kumekuwa na kukimbiakimbia kwenda kueleza mafanikio ya serikali kwa wananchi.
Naomba niseme hapa, Mawaziri wote wanatakiwa kushiriki kwenye vipindi hivi. Kwa wale ambao ni wapya wapo Makatibu wakuu na watendaji wengine wanaofahamu nini kimefanyika kwenye wizara zao, wawasaidie mawaziri kufanikisha hili,” alisema Samia.
Aliwataka Makatibu Wakuu, Naibu Makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Mabalozi walioteuliwa kwenda kuwa watumishi wa watu badala ya kuwa watawala na aliwataka wafikiri kwanza kabla ya kuamua jambo wanalolifanyia uamuzi ili kulinufaisha taifa.
Spika wa Bunge, Job Ndugai mbali ya kuwapongeza viongozi hao walioapishwa alisema dhamana waliyopewa ni kubwa na kwamba matarajio ya wananchi kwao ni makubwa. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, alisema wakuu wa mikoa ni wadau muhimu katika sheria, kwani ni wenyeviti wa Kamati za Maadili za Mikoa na hivyo wana wajibu wa kusimamia maadili ya viongozi wote mikoani mwao.
IMEANDIKWA NA REGINA MPOGOLO - habarileo