Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwaelekeza wakulima wa pamba kijiji cha Msai
wilayani Iramba, vipimo vya kati ya tuta na tuta, shimo na shimo kwa kutumia kamba na vijiti ili waweze kupanda kitaalamu na kuvuna kwa wingi.Picha na Libeneke la Kaskazini blog
Wakulima wa pamba kijiji cha Msai wilayani Iramba, wakishiriki kwa vitendo mafunzo yya kupima
urefu kati ya tuta na tuta, shimo na shimo kwa kutumia kamba na vijiti ili waweze kupanda kitaalamu na kuvuna kwa wingi.
Katibu Tawala Wilaya ya Iramba Pius Songoma akishiriki kuwaelekea wakulima wa pamba kijiji cha Msai
wilayani Iramba, vipimo vya kati ya tuta na tuta, shimo na shimo kwa kutumia kamba na vijiti ili waweze kupanda kitaalamu na kuvuna kwa wingi.
Konyo Mjika ambaye ni mkulima hodari wa pamba wilaya ya Iramba kutoka kijiji cha Msai akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida kwa zawadi ya kilo tano za mbegu ya pamba aliyopewa.
Zakaria Marko Mwakilishi wa Kampuni ya Biosustain itakayosambaza mbegu za pamba tani 300 mkoani Singida
akizungumza na wakulima wa zao hilo Katika kijiji cha Msai Wilayani Iramba.
*****
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iramba Emmanuel
Luhahula, asimamie kuvunjwa kwa bodi ya Ushirika wa Kijiji cha Msai Wilayani Iramba ndani ya wiki mbili, kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa zaidi ya shilingi
milioni 50.
Dkt Nchimbi ametoa agizo hilo mwishoni mwa wiki iliyopita katika mkutano na wakulima wa Pamba wa
Kijiji cha Msai, ambao wamemueleza kutokuwa na imani na viongozi wa bodi hiyo kutokana na upotevu wa fedha hizo na wakiwa hawajachukuliwa hatua yoyote.
Wakulima hao walimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa fedha zaidi ya milioni 50 zilitolewa na seikali kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la ghala la ushirika wa kijijini hapo lakini hakukuwa na ujenzi wowote uliofanyika huku wakifuatilia hawapewi majibu sahihi.
Walisema wana ushirika walijitahidi kutuma mwenyekiti wa Kijiji hicho kufuatilia upotevu huo bila mafanikio jambo lililowakatisha tamaa ya kuendelea na ushirika.
Dkt Nchimbi ali sema “moja ya Mhimili wa mafanikio ya kilimo cha pamba ni ushirika ulio imara, tunakoelekea
kwenye kilimo cha pamba chenye tija hawa wasiowaaminifu kwenye bodi watatukwaza na kutukwamishwa, kama bodi haifanyi kazi vizuri kwanini iendelee?, Mkuu wa
Wilaya nina imani kwa utendaji wako mzuri hili halitachukua zaidi ya wiki mbili”.
Aidha alimtaka Afisa Ushirika Mkoa wa Singida kusimamia na kutoa ushauri wa kitaalamu wakati wa kuvunjwa kwa bodi hiyo kwakuwa kazi ya mkoa ni kusuluhisha sio kutafuta maelezo marefu huku wananchi wanapotezewa muda.
“Afisa Ushirika hakikisha tarehe ishirini mwezi huu bodi hiyo iwe imeivunjwe na kuundwa bodi mpya ambayo itasimamia ushirika kwa umakini ili kuinua kilimo cha pamba Iramba”, alisisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha Dkt Nchimbi aliwatoa hofu wakulima kwakuwa mbegu aina ya UKM 08 za manyoya pamoja na viuatilifu zitafika
na kusambazwa kwa wakati huku akiwataka kupanda kitaalamu ili kwa ekari moja iwe na miche elfu 22 na mkulima avune zaidi ya kilo elfu moja za pamba.
Pia aliwaagiza
maafisa ugani wote kulima pamba ili mashamba yao yawe mashamba darasa, huku wakitakiwa kuhakikisha hakuna makosa katika hatua yoyote kuanzia kwenye kuandaa
mashamba, kupanda na kwenye upuliziaji dawa, bila kusahau kutoa taarifa kwa wananchi katika kila hatua.
Dkt Nchimbi amewapa wakulima hodari wawili wa zao la pamba zawadi ya kilo tano kwa kila mmoja kama
kianzio huku akiwaahidi kuwa mbegu za kutosha na viuatilifu kwa ajili ya maeneo yao watapatiwa.
Akisistiza kauli mbiu ya Singida mpya kwa pamba yenye tija aliwataka Wanasiasa, watendaji wa serikali na viongozi wa dini washirikiane na serikali kwa pamoja katika kutoa hamasa na elimu ya kilimo cha pamba.
Dkt. Nchimbi alitoa onyo kwa wauza pembejeo na wasambaaji wasio waaminifu ambao husambaza dawa
zisizo halisi kuwa serikali itawabaini na kuwapa adhabu kali huku akiwataka wakulima wasinunue dawa bila ushauri wa maafisa ugani.
“Kuna dawa nyingine ukipuliza kwenye wadudu waharibifu wa pamba badala ya kufa wananenepeana, sasa
ole wako serikali ikukamate wewe unayemuuzia
mwananchi dawa feki hakika tuakushughulikia ipasavyo”, amesisitiza Dkt.
Nchimbi.
Kwa upande wake Konyo Mjika ambaye ni mkulima hodari wa pamba wilaya ya Iramba kutoka kijiji cha Msai
alisema msimu wa mwaka jana amelima ekari nane na kupata kilo elfu sita ambapo ameweza kujenga nyumba nne za bati, kununua ng’ombe kadhaa na kuhudumia familia
yake.
Mjika aliongeza kuwa ameweza kuvuna pamba nyingi kutokana na kusikiliza ushauri wa wataalamu wa kupanda kwa kufuata mistari, kuweka mbolea na viuatilifu mapema.
Kutokana na mafanikio hayo Mkulima Mjika amesema kwa msimu huu anatarajia kulima ekarini shirini
pamoja na kuwashauri wanakijiji wenzake walime pamba kwa wingi huku wakifuata ushauri wa wataalamu ili waweze kuvuna kwa wingi.
Naye Zakaria Marko Mwakilishi
wa Kampuni ya Biosustain inayojihusiha na kilimo cha zao la pamba kwa mkataba alisema kwa msimu huu kampuni hiyo itasambaza mbegu za pamba tani 300 mkoani Singida.
Marko ameongeza kuwa uzalishaji wa pamba mkoani Singida umekuwa mdogo ukilinganisha na mahitaji ya
kiwanda chao ambapo mwaka jana zilipatitana kilo milioni 1 na mwaka huu zikaongezeka hadi kilo milioni 1.5 kutokana na jitihada za wakuu wa wilaya, Mkuu wa Mkoa na
viongozi mbalimbai.
Aliongeza kuwa Kijiji cha Msai chenye wakulima wa pamba zaidi ya mia tano wameweza kuzalisha kilo laki
tano huku wilaya ya Iramba yote ikizalisha kilo laki nane na nusu kwa msimu wa mwaka jana na mategemeo yakiwa makubwa zaidi kwa mwaka huu.
Marko alisema
kutokana na msukumo wa serikali na Viongozi wa Mkoa wa Singia ni matarajio yake kiwanda cha Bio Sustain sasa kitazalisha kwa faida kutokana na kupata pamba ya
kutosha hapa Singida na sio kuifuata mikoa ya jirani kama ilivyokuwa hapo awali.
Habari ,picha na Libeneke la Kaskazini blog