SHIRIKA la Kivulini (Women’s Rights Organization) lenye makao yake jijini Mwanza limeadhimisha "Siku ya Mtoto wa Kike" kwa kuendesha mafunzo ya siku moja ya Sheria na Sera dhidi ya ukatili kwa wanamabadiliko kutoka kata za Nyida na Itwangi wilayani Shinyanga.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Oktoba 11,2017 katika ukumbi wa Empire Hotel Mjini Shinyanga ambapo washiriki wa mafunzo hayo wametoka kwenye vijiji vitatu vya Nduguti, Butini na Nyida vilivyopo kwenye kata mbili za Nyida na Itwangi wilayani Shinyanga.
Mafunzo hayo yalilenga kuwapa washiriki uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na vitendo vya ukatili na baadhi ya sheria zinazotumika katika kuwaadhibu watu wanaotenda vitendo hivyo hasa dhidi ya wanawake na watoto na mbinu watakazotumia ili waweze kuisaidia jamii iachane na vitendo vya ukatili.
Miongoni mwa sheria ambazo wameshiriki wameelimishwa kuwa ni pamoja na Sheria ya ndoa (aina za ndoa, sifa na wajibu wa wanandoa, utaratibu wa talaka, ndoa za utotoni na madhara yake), Sheria ya Ardhi (Haki ya mwanamke kumiliki ardhi), Sheria ya makosa ya kujamiiana na Mirathi na utaratibu wa mirathi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Mwezeshaji katika mafunzo hayo Glory Mlaki ambaye ni Ofisa mipango Shirika la Kivulini alisema pamoja na dini kumtambua mwanaume kama kichwa na mkuu wa familia ni vyema wakatumia vyema fursa hiyo akiwashauri wanaume kujiepusha na tabia ya kutoa vipigo kwa wanawake kwa kigezo tu cha kwamba wao ndiyo vichwa ndani ya familia.
Hata hivyo alisema inapotamkwa neno, Ukatili wa kijinsia haina maana ya kuwalenga wanawake au watoto peke yao bali ieleweke kuwa wapo pia wanaume wanaotendewa vitendo vya ukatili japo baadhi yao huona aibu kulalamika hadharani.
“Kwa hali hii basi ni vizuri jamii ikatafuta suluhu nyingine ya kutatua matatizo ndani ya familia badala ya kutumia njia ya vipigo ambayo ina madhara makubwa kwa anayetendewa hii ni pamoja na akinamama kujiepusha na mazoea ya kuwachapa viboko watoto wao, maana huu nao ni ukatili”,alieleza.
Alifafanua kuwa daima ukatili unafanyika kijinsi, kuna wanawake pia wanafanya ukatili dhidi ya wanaume lakini pia takwimu zinaonesha wanawake ndiyo wanaoongoza kwa kutendewa ukatili na wanaume.
Hata hivyo aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kutojaribu kujibu vitendo vya ukatili kwa kufanya ukatili badala yake wajitahidi kutoa elimu kwa jamii iweze kuacha kuwafanyia ukatili watu wengine ama kuwaadhibu watoto wao kwa makosa ya watu wengine.
Mlaki pia aliwaelimisha washiriki juu ya maana ya dhana ya ndoa kwa kusema, Sheria ya ndoa ya mwaka 1971 katika kifungu cha 160 inaeleza juu ya mahusiano kwamba endapo mwanamke akiishi na mwanaume kwa miaka miwili au zaidi mfululizo na jamii inayowazunguka ikawatambua na kuwapa hadhi ya mume na mke, basi mahusiano hayo yaweza kupata dhana ya kuchukuliwa kama wanandoa.
Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo walikiri kuwepo kwa tatizo la ndoa za utotoni katika vijiji vyao ambapo walishauriwa kuzipiga vita na badala yake wahakikishe watu wanaofunga ndoa ni wale waliofikia umri wa utu uzima wenye umri wa miaka 18.
Walisema baadhi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaendelea kufanyika kutokana na baadhi ya jamii kuendeleza kuamini mila na desturi ambazo baadhi yake zimepitwa na wakati.
Aliwataka Wanamabadiliko wawe mstari wa mbele katika kuielimisha jamii ili iweze kuachana na mila na desturi zilizopita na wakati ili kuweza kumpa mtoto wa kike fursa sawa ya kupata elimu na haki nyingine kama anavyopatiwa mtoto wa kike.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Afisa miradi msaidizi kutoka Shirika la Kivulini Vaileth Elisa.akisikiliza hoja kutoka kwa mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo.
Mwezeshaji ambaye ni Ofisa mipango kutoka Shirika la Kivulini, Glory Mlaky akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya Sheria dhidi ya Ukatili kwa wanamabadiliko.
Mmoja wa wawezeshaji kutoka Shirika la Kivulini, Olpha Maduhu akitoa maelezo ya utangulizi kwa washiriki wa mafunzo.
Akina mama pia hawakuwa nyuma katika uchangiaji wa mada. Hapa Elizabeth Mayunga kutoka kijiji cha Butini kata ya Itwangi akichangia maoni yake kwenye mada ya Jinsi na Ukatili wa kijinsia.
Mwezeshaji Glory Mlacky akiandika hoja za washiriki.
Wawezeshaji kutoka Shirika la Kivulini wakijadiliana jambo, kutoka kushoto ni Eunice Mayengela, Olpha Maduhu na Vaileth Elisa.
Washiriki wakiwa makini katika kuchukua kumbukumbu muhimu za mafunzo.
Mazoezi ya viungo yakiendelea kama sehemu ya mafunzo
Picha zote na Suleiman Abeid - Mtetezi wa haki blog na Malunde1 blog