Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameanza kuzungushwa katika vituo vya Polisi jijini Dar es Salaam.
Zitto baada ya kuhojiwa katika Kituo cha Polisi cha Chang’ombe mkoani Temeke sasa amehamishiwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Ado Shaibu amesema baada ya Zitto kuhojiwa kuhusu aliyozungumza kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni za udiwani zilizofanyika Kijichi Jumapili Oktoba 29,2017 aliachiwa kwa dhamana.
Shaibu amesema Zitto aliyewakilishwa na wanasheria Venance Msebo na Steven Mwakibolwa alidhaminiwa na watu wawili na alitakiwa kurudi kituoni hapo Jumatatu Novemba 6,2017. Hata hivyo, amesema alikamatwa tena.
Akizungumzia kukamatwa kwa Zitto, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa wanamshikilia kwa lugha za uchochezi.
"Tunamshikilia kwa uchochezi na kutoa lugha zisizo na staha na yupo Central hapa,'' amesema Kamanda Mambosasa