Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita Daniel Limbe
Habari kutoka mkoani Geita zinaeleza kuwa waandishi wa habari wanne mkoani humo wameshambuliwa kwa bakora na kuwekwa sero na askari wa jeshi la polisi mkoani Geita wakati wakitekeleza majukumu yao baada ya wanafunzi wa shule ya sekondari Geita kufanya vurugu shuleni.
Inaelezwa kuwa waandishi hao wamekutwa na maswahibu hayo jana Oktoba 21,2017 ambapo mbali na kupigwa kamera ya mwandishi wa habari Esther Sumira wa Azam Tv imeharibiwa.
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita Daniel Limbe amewataja miongoni mwa waandishi wa habari waliokumbwa na kadhia hiyo kuwa ni Esther Sumira ( Azam Tv) ,Editha Edward (Mtanzania,Rehema Matowo(Mwananchi) na Emmanuel Ibrahim (Clouds Media).
Taarifa zinasema hakuna uhusiano mzuri baina ya jeshi la polisi mkoa wa Geita na waandishi wa habari.
HILI HAPA TAMKO LA KLABU YA WAANDISHI WA HABARI MKOA WA GEITA KULAANI TUKIO LA WAANDISHI WA HABARI KUPIGWA
Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Geita (GPC) kinalaani vikali tukio la waandishi wa habari kushambuliwa kwa kipigo na jeshi la polisi wakati wakitekeleza majukumu yao kwenye vurugu zilizotokea jana kwenye shule ya sekondari Geita(Geseco).
Vurugu hizo ambazo wanafunzi walikuwa wakishinikiza Bodi ya shule kuhakikisha inakwenda kufanya mazungumzo ya haraka na jeshi la polisi ili kuwatoa mahabusu wanafunzi watano waliokuwa wakishikiliwa kwa madai ya kumjeruhi kwa kipigo mwanafunzi mwenzao wa kidato cha tano,walitumia mawe kuponda majengo ya shule na kutishia kuichoma moto shule hiyo iwapo hatua za makusudi za wenzao kulejea shuleni hazitafanikiwa.
Baada ya vurugu hizo waandishi walifika eneo la tukio kwa ajili ya kutimiza wajibu wao ambapo Mwandishi wa gazeti Habari Leo,Editha Edward,alikumbana na kichapo cha askari polisi waliofika kutuliza ghasia zilizokuwa zimejitokeza shuleni hapo licha ya kujitambulisha kuwa yeye ni mwandishi wa habari.
Wengine waliokumbana na Kadhia hiyo ni Rehema Matowo, mwandishi wa gazeti la Mwananchi ambaye alinyang'anywa simu yake na kuwekwa chini ya ulinzi kwa muda kwenye chumba cha walinzi wa shule hiyo kabla ya kumrejeshea simu yake na kumwachia huru huku akitakiwa aondoke eneo hilo.
Hata hivyo Mwandishi wa Azam Tv Ester Sumira,alinyang'anywa kamera yake na walimu wa shule hiyo kwa muda wa zaidi ya dakika 20 wakimtaka kutochukua picha za vurugu zilizokuwa zikiendelea eneo hilo.
Na Mwandishi wa Cloud Tv,Emmanuel Ibrahimu alikumbana na msukosuko baada ya polisi kuzuilia pikipiki yake na kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kazi.
Kutokana na vitendo hivyo visivyokuwa vya kiungwana ambavyo vinakiuka misingi ya utawala Bora na Haki za Binadamu,Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Geita kinaendelea kulaani vikali na tunaziomba taasisi zingine kama UTPC,MCT, TEF na wadau wote kulaani vitendo hivi vya kihuni ambavyo vinaendelea kutamalaki kila uchwao na kuharibu taswira nzima ya Utawala bora nchini.
Hata hivyo hatua zaidi zitakazochukuliwa na uongozi wa Klabu zitatolewa kesho baada ya kikao cha waandishi wa habari.
Limetolewa na Daniel Limbe,mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Geita.
MSIKILIZE HAPA MWENYEKITI WA GEITA PRESS CLUB,DANIEL LIMBE AKIELEZEA KUHUSU TUKIO HILO WAKATI AKIZUNGUMZA NA MALUNDE1 BLOG