Chuo kikuu kimoja kaskazini magharibi mwa Nigeria kimeanza kuwaajiri wachezea nyoka kama njia ya kupunguza hatari ya watu kuumwa na nyoka wakiwa chuoni.
Zainab Umar, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika chuo kikuu hicho cha Umaru Musa Yar'Adua katika jimbo la Katsina, alifariki wiki iliyopita baada ya kuumwa na nyoka.
Mkuu wa masuala ya wanafunzi chuoni Dkt Suleiman Kankara amesema wachezea nyoka wamewahi kuajiriwa awali baada ya taarifa za watu kuumwa na nyoka.
Utamaduni huo ni maarufu sana mataifa ya Asia kusini, na pia baadhi ya maeneo ya Afrika.
Bi Umar aliondolewa kwenye kliniki ya chuo hicho alipokuwa akipokea matibabu kinyume na ushauri wa madaktari.
Alihamishwa na marafiki zake na nduguye.
Wachezea nyoka hucheza ala ya muziki, sana filimbi au zumari, na nyoka huonekana kana kwamba wanatulizwa au kuathiriwa na wimbo unaochezwa hata wakiwa karibu sana.
Jambo linaloshangaza wengi ni kwamba nyoka huonekana kubadilishwa nia na wimbo wa wachezea nyoka hata wakiwa karibu sana kushambulia.
Nchini Nigeria, wachezea nyoka huwashika hata swila kwa mikono yao wakicheza nao hadharani na wakati mwingine huwashirikisha watu wanaohudhuria.
Chanzo-BBC