Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewatangazia kiama wafanyakazi wa TANESCO nchini watakaoshirikiana na watu kuiba miundo mbinu ya umeme, ili kuhakikisha huduma hiyo haihujumiwi kama zingine.
Dkt. Kalemani ameyasema hayo jana alipokuwa akiongea na maafisa wa TANESCO, na kusema shirika limekuwa likipoteza mapato makubwa kufuatia umeme unaopotea, kutokana na kuhujumiwa miundo mbinu yake, na wizi wa umeme uliokithiri unaofanywa na baadhi ya wateja.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya TANESCO kugundua wateja zaidi ya mia moja wanatumia umeme bila kulipia hali inayolitia hasara shirika, baada ya kufanya operesheni maalum ya kukagua watu wanaoiba umeme jijini Dar es salaam.
Kufuatia operesheni hiyo, baadhi ya watu wamekuwa wakiyakimbia makazi yao kuogopa kutiwa mikononi mwa polisi, na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.