WCF YAWAJENGEA UWEZO KWA WAGANGA NA MADAKTARI KANDA YA ZIWA

Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF umetoa semina kwa Waganga na Madaktari Kanda ya Ziwa ili kuwajengea uwezo wa kufanya tathmini sahihi kwa wafanyakazi wanaoumia kazini kwa ajili ya kulipwa fidia.

Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Masha Mshomba amesema ujio wa mfuko huo ni faraja kwa waajiri na waajiriwa kwani umelenga kuondoa kero walizokuwa wakizipata wafanyakazi baada ya kuumia kazini hivyo semina hiyo itasaidia madaktari hao kufanya tathmini za malipo kwa haraka zaidi.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa semina hiyo, amewasihi waajiri wote kujiunga na mfuko huo na kwamba ni kosa kisheria kwa waajiri wanaokwepa kujiunga na kutoa michango kwa ajili ya waajiriwa wao.

Dkt.Furaha Munema kutoka hospitali ya Rufaa mkoani Mwanza Sekou Toure ambaye ni mmoja wa
madaktari walionufaika na semina hiyo ya siku tano kuanzia leo, amebainisha kwamba itawasaidia kutenda haki wakati wa tathmini kwa mfanyakazi atakayekuwa
ameumia kazini.

Naye mmoja wa wawezeshaji wa semina hiyo Dkt.Robert Mhina ambaye ni daktari bingwa upasuaji mifupa kutoka hospitali ya taifa Muhimbili kitengo cha mifupa MOI, amesema mfuko wa fidia WCF umesaidia kuondoa usumbufu uliokuwepo hapo awali baada ya wafanyakazi kuumia kazini.

Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF unatoa huduma ya matibabu, malipo ya ulemavu wa muda, ulemavu wa kudumu, malipo kwa anayemhudumia mgonjwa, msaada wa mazishi, malipo kwa wategemezi ikiwa mfanyakazi atafariki dunia, ukarabati pamoja na ushauri nasaha.
Mgeni rasmi, Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Mongella (katikati), akiwa pamoja na viongozi wa WCF. 
Baadhi ya Waganga na Madaktari wanaoshiriki semina hiyo katika ukumbi wa Benki Kuu BOT Jijini Mwanza.



Na Binagi Media Group

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post