Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amekabidhi rasmi Hospitali za Rufaa za Mikoa kwa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Hatua hiyo imekuja kufuatia pendekezo lililotolewa na Rais John Magufuli Novemba 25 aliyetaka hospitali hizo zitolewe TAMISEMI ziwe chini ya Wizara ya Afya ili kuweza kuwapo kwa mfanano wa sera lakini pia ugawaji wa rasilimali watu katika hospitali hizo.
Rais aliyasema hayo alipokuwa akizindua Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Kampasi ya Mloganzila na kueleza kuwa kumekuwa na utofati mkubwa wa ugawaji wa madaktari katika hospitali za rufaa kutokana na mgawanyo huo kufanywa na wizara mbili tofauti.
Mbali na Rais kuagiza hospitali hizo ziwe chini ya Wizara ya Afya ili zisimamiwe vizuri na wataalamu na pia ameiagiza wizara hiyo kurekebisha mgawanyo wa madaktari katika hospitali zote nchini ili kuepuka uwepo madaktari wengi katika sehemu moja, huku maeneo mengine yakiwa na uhaba mkubwa.
“Kuanzia leo (Novemba 27) hospitali zote za rufaa zitakuwa chini ya Wizara ya Afya na kwetu sisi (TAMISEMI) tutabaki na hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati pekee,” amesema Waziri Jafo.
Kuhusu madaraka ya Waganga Wakuu wa Mikoa amesema wataendelea kuwa chini ya TAMISEMI lakini Waganga Wafawidhi wa Hospitali watapelekwa Wizara ya Afya.