Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ALIYEKUWA AKIJIITA RIPOTA WA STAR TV NA MTOTO WA KAMANDA KOVA ATUPWA JELA MWAKA MMOJA KWA UTAPELI

Aliyekuwa akijita Ripota wa STAR TV wa mkoa wa Katavi na mtoto wa Kamanda Suilemani Kova anayejulikana kwa jina la Gerald Kova mkazi wa mkoa wa Mwanza amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya utapeli na kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu.



Hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Mpanda Marko Pagyo baada ya Mahakama kulidhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka.


Mwendesha mashtaka wa jeshi la Polisi WP Salima alidai Mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo hapo Februari 8 mwaka huu katika eneo la Hotel ya Madina Manispaa ya Mpanda.

Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo ambaye alikuwa anajitambulisha kuwa ni mwakilishi wa STAR TV yenye Makao yake makuu Mkoani Mwanza na ni mtoto wa Kamanda Selemani Kova alijipatia kwa njia ya udanganyifu Kamera moja aina ya Canon yenye thamani ya Tshs 3,500,000/= ,Laptop moja na stendi ya Kamera ya video mali ya Elias Mlugala.


Alisema mtuhumiwa baada ya kuwa amejipatia mali hizo kwa njia ya udanganyifu aliondoka Mpanda na kutokomea kusikojulikana huku akiwa ametapeli kamera nyingine  Kibada aina ya Nikon D 7,200 kwa Ernest mali ya Chama cha Wandishi wa Habari Mkoa wa Katavi yenye thamani ya Tshs 4,900,000.


Mwendesha mashtaka huyo aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa baada ya kutokomea haikujulikana alikokuwa amekimbilia mpaka hapo mwezi Agosti alipokamatwa huko Kahama mkoani Shinyanga na huko alikuwa ajitambulisha kwa jina la Crispin Masawe na alikamatwa baada ya kufanya utapeli mwingine wa kujipatia kwa njia ya udanganyifu Laptop moja ya mwandishi wa habari wa Kahama.

Alidai kuwa baada ya kukamatwa alifikishwa katika mahakama ya Mwanzo ya Kahama na kuhukumiwa kifungo cha miezi mitatu au kulipa faini ya Tshs 100,000 hata hivyo hakuweza kulipa na alikwenda gerezani.

Mwendesha mashtaka alieleza ndipo Elias na Kibada walitoa taarifa kituo cha polisi cha Mpanda juu ya mtuhumiwa wao kuhukumiwa kifungo hivyo walifanya utaratibu na waliweza kwenda Kahama na kumlipia faini hiyo na kumtoa gerezani na kisha akawa chini ya ulinzi wa polisi na aliweza kusafirishwa hadi Mpanda na ndipo alipofikishwa Mpanda na Polisi alipoonyesha vifaa vyote ambavyo alikuwa amemuuzia mfanya biashara mmoja wa huko Maji Moto Wilayani Mlele mkoani Katavi.

Mshtakiwa Gerald Kova katika utetezi wake kabla ya kusomewa hukumu aliiomba Mahakama imwachie huru kwa kile alichodai kuwa anasumbuliwa na magonjwa pia mama yake mzazi ni mgonjwa na anamtegemea yeye.

Baada ya utetezi huo hakimu Paragyo alisoma hukumu na kuamuru mshitakiwa atumikie kifungo cha mwaka mmoja jela na pindi atakapotoka gerezani atatakiwa kulipa Tshs 800,000.

Mshitakiwa huyo anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani hapo kwa ajiri ya kesi ya pili inayomkabili ya kujipatia kamera Nicon mali ya chama cha waandishi wa habari mkoa wa Katavi ambapo kesi hiyo itaendelea kusikilizwa.

Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com