BABA CCM ATAKA MWANAWE ASICHAGULIWE UDIWANI



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kwa kishindo kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Udiwani katika Kata ya Kimala wilayani Kilolo mkoani Iringa huku Barthoromeo Kisoma, baba mzazi wa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), akipanda jukwaani na kuwataka wapiga kura wa kata hiyo wasimchague mwanaye.

Wakati CCM inawakilishwa katika uchaguzi huo na Amoni Kikoti, mkazi wa Kijiji cha Uruti, Chadema imemsimamisha Tumson Kisoma aliyehamishia makazi yake Iringa Mjini.

 Baba mzazi wa mgombea huyo wa Chadema alitoa rai hiyo baada ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kilolo, Kilian Myenzi kumnyanyua katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni hizo za CCM zilizofanyika juzi katika Kijiji cha Kimala na kumtaka kuwasalimia wananchi.

“CCM oyeeeeeee, CCM oyeeeee,” alisema mzazi huyo na kuwafahamisha wananchi waliofurika katika mkutano huo kwamba mgombea wa Chadema ni mwanawe, lakini hana uwezo wa kuwawakilisha wananchi wa kata hiyo.

Kisoma alisema kata hiyo inahitaji maendeleo ya kweli na mahali pekee pa kuyapata ni kupitia CCM, hivyo kuomba wapiga kura wamchague mgombea wa CCM, Amoni Kikoti.

Awali Myenzi ambaye pia ni sehemu ya familia ya Kisoma alisema Kata ya Kimala inahitaji diwani wa CCM ili kutengeneza mnyororo mzuri wa mawasiliano na Serikali ya CCM.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Christopher Magala aliwaomba wapiga kura wa kata hiyo kujihadhari na matapeli wa kisiasa wanaobadili rangi za hoja zao kila kukicha.

 “Kabla Rais Magufuli haijaingia madarakani hoja zao zilikuwa rushwa, ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma na nyingine nyingi.

Baada ya hayo yote kuanza kushughulikiwa katika awamu hii ya uongozi, wamebadilika sasa wanatetea watu wanaojihusiha na vitendo hivyo, nchi haihitaji viongozi wa aina hiyo,” alisema Magala.

Naye Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia Wilaya ya Mufindi, Iringa , Jamhuri William alisema; “sioni ni kwa namna gani, wananchi wa kata hii mtamchagua mgombea kutoka katika chama kilichoshindwa vibaya katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.”

Aidha kada maarufu wa CCM, Asia Abdalla alisema Kikoti atashinda kwa kishindo kwa sababu wapiga kura wanajua mengi yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na Serikali.

 Abdalla ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, alitaja miradi ya maendeleo ambayo Serikali ya CCM imeitekeleza katika miaka miwili iliyopita na akasema mengi yanakuja.

Akimwombea kura, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto alisema; “Kikoti ana sifa za kuwa msaidizi wangu kwani ni mwadilifu, mwaminifu na mchapakazi, mchagueni.”

 Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Zainabu Mwamwindi alisema Kata ya Kimala ni kata iliyoongozwa na CCM kwa miaka yote itakuwa miujiza kama watakengeuka.

Chanzo - Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post