Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CCM YAMTANGAZA KITILA MKUMBO KUWA MWANACHAMA WAO,SIKU 39 BAADA YA KUJIVUA ACT WAZALENDO



Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemtangaza Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo amejiunga na chama hicho.


Uamuzi huo wa Profesa Mkumbo kujiunga na CCM ameufanya ikiwa ni siku 39 zimepita tangu alipotangaza kujivua uanachama wa ACT- Wazalendo Oktoba 9.


Taarifa ya CCM aliyoitoa mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Singida, Martha Mlata imesema chama hicho Mkoa wa Singida wanamkaribisha kwa mikono miwili ili waendelee kuimarisha chama katika mkoa huo.


“Nina furaha kuwatangazia wanachama na wapenzi wa CCM Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujuma kuwa…Profesa Kitila Mkumbo amejiunga tena na chama chetu,” amesema Mlata na kuongeza:


“Ni fursa kubwa kwa mkoa kumpokea mwalimu baada ya kumpoteza mwanafunzi siku chache zilizopita.”


Akifafanua zaidi katika mazungumzo na Mwananchi baada ya kutoa taarifa hiyo, Mlata amesema “Profesa Mkumbo amejiunga wiki moja iliyopita na amelipita ada yote aliyokuwa akidaiwa katika kipindi chote na na mimi nilichokifanya ni kuwajulisha tu wanachama wetu kuwa mwana mpotevu karudi nyumbani.”


Alipoulizwa kama ni njia ya kwenda kugombea ubunge wa Singida Kaskazini amesema “hapana, pale kuna vijana wengi sana ambao wako tayari kuwatumikia wananchi, kwanza hawezi kuacha madaraka makubwa aliyopewa na mheshimiwa Rais, yeye ameamua tu kurudi nyumbani.”


Kuhusu kujiunga CCM huku akiwa mtumishi wa umma, Mlata ambaye ni mbunge wa viti maalum wa chama hicho amesema hilo halina tatizo kwani hata alipokuwa ‘uhamishoni’ bado alijipambanua ni mwanachama wa chama fulani kwa hiyo kurejea nyumbani si kosa.

Imeandikwa na Ibrahim Yamola, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com