Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kina uhakika wa kushinda uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo la Singida Kaskazini ambalo Bunge lilitangaza jana kuwa liko wazi baada ya aliyekuwa Mbunge wake kujiuzulu mapema wiki hii.
Afisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alipoulizwa kuhusu uchaguzi huo, alisema watamtangaza mgombea wake, baada ya Nec kutangaza kuhusu uchaguzi huo.
"Tutamtangaza mgombea wetu ambaye tutamsimamisha kwenye uchaguzi huo mdogo na tunaamini tutakayemsimamisha lazima atashinda," alisema Makene.
Aidha kwa upande wa Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima baada ya kuulizwa iwapo amekwishapata barua kutoka bungeni na lini itatangaza uchaguzi mdogo wa jimbo hilo, alifunguka na kudai kuwa muda ukifika watatoa taarifa.
Kutangazwa kuwa wazi kwa jimbo hilo, sasa kunatoa fursa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza mchakato wa kupata mrithi wa Lazaro Nyalandu ambaye alitangaza kujizulu nafasi hiyo na kujitoa uanachama wa CCM mwanzoni mwa wiki.
Taarifa iliyotolewa jana ilisema Spika wa Bunge, Job Ndugai, amemwandikia Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage, kumfahamisha kuwa jimbo hilo liko wazi.
Taarifa ya Bunge ilisema Spika ameandika barua hiyo kwa mujibu wa kifungu 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura ya 343, ya mwaka 2015) kinachoelekeza kwamba, pale ambapo Mbunge atajiuzulu, atakufa au sababu nyingine yeyote tofauti na zilizoainishwa katika kifungu cha 113, Spika atamjulisha Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kutangaza kwenye Gazeti la Serikali kwamba kiti hicho cha Ubunge kiko wazi.
Jumatatu ya wiki hii, Nyalandu alitangaza kujiuzulu nafasi ya Ubunge na kutangaza kukihama Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutaja sababu za kuchukua uamuzi huo kuwa ni kutoridhishwa na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za kibinadamu na ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya watanzania.