Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIWANI WA CCM ATUPWA JELA MIAKA MITATU



Mahakama ya Wilaya ya Mlele mkoani Katavi imemhukumu  kifungo cha miaka mitatu jela diwani wa kata ya Katumba (CCM) wilayani humo, Seneta Jeris Baraka (32) baada ya kupatikana na hatia ya kuomba na kupokea rushwa ya Sh500,000/-

Akisoma hukumu hiyo jana, hakimu wa mahakama hiyo , Tetimus Swai alisema kuwa mshtakiwa alitiwa hatiani kwa makosa mawili ya kuomba rushwa ya Sh 1,000,000/- na kupokea rushwa ya Sh 500,000/- kutoka kwa mfugaji aitwae Charles Kiligiwa maarufu kama Mange .

Alisema mshtakiwa huyo katika kosa lake la kwanza atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh 500,000/- na katika kosa la pili atatumikia kifungo cha miaka mitatu bila faini.

“Hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu jela bila kulipa faini na haki yake ya kukata rufaa iko wazi", alihukumu Swai.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Tassisi ya Kupambana na Kuzuia Rukwa (Takukuru) , Bahati Haule alidai mahakamani hapo kuwa Mahakama ya Mwanzo katika Kambi ya Wakimbizi wa Burundi ya Katumba ilimuamuru mfugaji Kiligiwa maarufu Mange atoe mifugo yake yote aliyoiingiza kambini humo kinyume cha sheria.

Aliongeza kuwa ndipo mshtakiwa alimshawishi mfugaji huyo ampatie kiasi cha Sh 1,000,000/- ili asitekeleze amri hiyo iliyotolewa na mahakama hiyo kwamba asiitoe mifugo yake kambini humo.

Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka Haule mfugaji huyo alimpatia mshtakiwa huyo kiasi cha Sh 100,000/- ikiwa ni malipo ya awali.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Mei , 11, mwaka jana mshtakiwa alimtaka mfugaji amlipe kiasi kilichobakia ,ndipo mtego uliwekwa kati ya maofisa wa Takukuru na mfugaji ambapo alimtaka mshtakiwa wakutane katika kijiji cha Ivyungwe amlipe kiasi cha Sh 400,000/ ili nusu iliyobakia amlipe siku za usoni.

Katika utetezi wake mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa ana familia na mama mazazi ambaye ni mzee sana wote wakimtegemea kwamba ni mara yake ya kwanza kushtakiwa mahakamani.

Na Walter Mguluchuma- Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com