Wanawake wanaopenda kutafuna udongo maarufu kwa jina la pemba na hasa wakati wa ujauzito wanapaswa kufikiria mara mbili kabla ya kufanya hivyo.
Hii ni kutokana na watafiti nchini kubaini kuwa viwango vya madini ya kemikali katika udongo huo nchini vimezidi kipimo kilichowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Utafiti uliofanywa katika mikoa 12 ya Tanzania na wanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Bugando (Cuhas-Bugando) wakishirikiana na wenzao kutoka Canada na Marekani, umebaini madini kama vile lead (risasi), arsenic, cadmium, nickel na aluminiamu katika udongo huo yanahatarisha afya za akinamama hao na watoto ambao hawajazaliwa.
Utafiti huo ambao umekamilika mwaka huu umefanywa kwa kipindi cha miaka mitano katika mikoa ya Singida, Rukwa, Lindi, Dodoma, Mbeya, Kusini Pemba, Mara, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro, Tanga na Ruvuma.
Hata hivyo, mtafiti mkuu katika utafiti huo, Elias Nyanza kutoka Cuhas amesisitiza kuwa wao wamejikita katika kuchanganua udongo unaouzwa katika masoko.
“Hatuna shida na uuzwaji wa udongo huu. Kinachotutia hofu ni viwango vya madini ya kemikali tulivyobaini na vyanzo vya udongo huo,’’ alisema Nyanza katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi.
“Tulichukua sampuli za udongo kutoka maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika mikoa 12 ya Tanzania. Tuliuchanganua udongo huo kwa kutumia utaalamu wa kimaabara uitwao ICP-MS.’’
Alisema utafiti huo uko katika mchakato wa kuchapishwa katika majarida ya kisayansi kimataifa.
“Tunashauri ulaji wa udongo huu uzuiwe hadi pale walaji watakapohakikishiwa usalama wao kiafya,’’ alisema Nyanza ambaye ni mtaalamu wa afya ya mazingira kutoka Shule Kuu ya Afya ya Jamii, Cuhas-Bugando. Nyanza alishirikiana na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Colorado Denver cha Marekani na cha Calgary, Canada. Alisema madini waliyoyabaini kama vile risasi, cadmium na arsenic tayari yameorodheshwa na shirika la Marekani la viambata vyenye sumu na magonjwa.
Mtafiti huyo alisema madini hayo yanajulikana kwa kusababisha madhara kiafya na hasa kwa mama na mtoto, hata yakiwa katika kiwango kidogo. “Madini mengi ya kemikali, hasa yale tuliyochanganua kutoka kwenye udongo unaoitwa pemba yako katika viwango vya juu kuliko inavyotakiwa katika miongozo ya Shirika la Afya Duniani,’’ alisema.
Nyanza alisema, “Kuna wanawake tulikuta wanakula udongo wenye viwango vya madini hayo kufikia 50 micrograms per litre hadi 60 micrograms per litre, lakini WHO inasisitiza kuwa madini haya yanakuwa salama pale yanapotumika katika viwango vya 10 micrograms per litre.’’
“Ulaji wa udongo huu unaongeza hatari ya wanawake kuzaa watoto wafu, wenye uzito mdogo, njiti na hata wakati mwingine kusababisha watoto kuzaliwa wakiwa na hitilafu za kimaumbile,’’ alitahadharisha Nyanza.
Mkemia mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyere amependekeza watafiti hao wachukue sampuli walizozipata katika utafiti na kuziwasilisha katika ofisi yake ili hatua za kuingilia kati suala la udongo huo zitekelezwe ipasavyo na mamlaka zinazohusika.
“Sisi katika maabara ya mkemia mkuu bado hatujafanya utafiti kama huo. Ila tuna teknolojia ya kuweza kubaini hicho wanachodai wamekuta katika udongo huo. Wataarifu walete sampuli walizokusanya ili nasi tujiridhishe kwanza,’’ alisema Profesa Manyere alipozungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake jijini Dar es Salaam kuhusu utafiti huo.
“Mojawapo ya madini yanayotajwa hapo ni risasi ambayo kweli ni hatari kwa afya. Sisi tuko katika mchakato wa kuyawekea miongozo lakini si katika ulaji wa udongo.”
Maeneo ya uchimbaji dhahabu
“Hatari zaidi tuliibaini kwa wanawake wanaokula udongo unaotengenezwa kutoka ardhi iliyopo maeneo ambayo kuna shughuli za wachimbaji wadogo wa dhahabu,’’ alisema Nyanza.
Mwaka 2014, utafiti mwingine uliofanywa katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji madini ulionyesha kati ya wanawake 115 walioshirikishwa, asilimia 69 walinunua udongo (pemba) huo kutoka kwenye maduka na asilimia 31 walikula udongo maarufu kama kichuguu. “Kwa pemba na kichuguu, utafiti huo uligundua viwango vikubwa vya arsenic, chromium, shaba, chuma, manganizi, nickel na zinki. Viwango vya cadmium na zebaki vilikutwa zaidi katika sampuli za kichuguu,’’ watafiti walisema katika Jarida la BMC Pregnancy and Childbirth utafiti ulikochapishwa.
Katika utafiti huo, watafiti walishauri hatua za kiafya zichukuliwe kunusuru afya za akinamama wanaokula udongo unaozalishwa kutoka maeneo ya migodi.
“Hatua za kisera na programu za kuelimisha zichuliwe katika mazingira ya wachimbaji wadogo, wanawake wanazidi kula udongo na wanajiweka katika hatari kiafya,’’ wanaeleza watafiti katika mapendekezo yao.
Pia, walisema sababu zinazowafanya wanawake kula udongo zichunguzwe na elimu itolewe katika kukabiliana na hatari za kiafya.
Wengi wanaamini ulaji wa udongo huwasaidia kutatua changamoto za ujauzito kama vile kichefuchefu, upungufu wa madini ya chuma na wakati mwingine wanakuwa na hamu tu ya kuula.
Dk Latifa Kalinga kutoka Hospitali ya Mkoa ya Songwe, alisema kwa uzoefu wake wa kidaktari na mwanamke aliyewahi kuwa mjamzito, kula udongo ni kati ya changamoto zinazowakumba wengi. “Ujauzito huwa na changamoto nyingi. Wakati mwingine wanawake hupenda tu kula udongo. Wanaweza kula hata barafu katika jokofu, kutafuna mchele kilo nzima na mengine. Hii tabia inaitwa pica katika lugha ya kitaalamu,’’ alisema huku akisisitiza inapaswa washauriwe waache kwa kujiweka katika hatari ya kupata minyoo inayosababisha upungufu wa damu
Imeandikwa na Syriacus Buguzi - Mwananchi Mwanza