Rais Uhuru Kenyatta akiwa na mwanafunzi bora kitaifa, Goldalyn Kakuya
****
MSICHANA mwenye ulemavu wa ngozi (albino) amesema ushindi wake wa kuwa namba moja kitaifa kwenye mtihani wa taifa wa kumaliza elimu ya msingi nchini Kenya (KCPE) ni ushindi wa albino wote na kwamba, hakuna anayeweza kutimiza ndoto zake bila alichoiita kuwa ni Ph.D yaani sala, juhudi na nidhamu.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu Kenya, mtoto huyo, Goldalyn Kakuya (14) amepata maksi 455 kati ya 500. Wanafunzi 993,718 walifanya mtihani huo. Mwaka jana mwanafunzi wa kwanza kitaifa alipata maksi 437.
Mbunge wa Kuteuliwa, Dk David Sankok aliwapongeza wanafunzi sita wenye ulemavu kwa kuwa miongoni mwa watahiniwa 100 bora kitaifa. “Leo sitaki tusheherekee kwa ajili yangu tu, nataka tusheherekee ualbino,” alisema Goldalyn.
Ijumaa iliyopita msichana huyo aliyekuwa akisoma kwenye Shule ya Mtakatifu Anne Junior iliyopo Lubao kwenye jimbo la Kakamega, alikwenda Ikulu ya Kenya kukutana na Rais Mteule, Uhuru Kenyatta na Naibu Rais mteule, William Ruto.
Kenyatta na Ruto walimpongeza Goldalyn kwa mafanikio aliyopata. Kenyatta aliahidi kumsaidia mtoto huyo atimize ndoto zake. Wakati akiwa hapo Ikulu na wazazi wake, msichana huyo alipata fursa ya kuzungumza na Rais Kenyatta na kumkumbatia kiongozi huyo.
“Nilimpongeza na nilizungumza na mwanafunzi bora wa mwaka huu KCPE Goldalyn Kakuya. Goldalyn ana mwelekeo mzuri sana wa maisha yake ya baadaye na utawala wetu utahakikisha kwamba anapata kila aina ya msaada anaohitaji kutimiza ndoto zake,” alisema.
Katika hafla hiyo, wazazi wa msichana huyo walikabidhiwa hundi ya Shilingi 100,000 za Kenya. Mama mzazi wa msichana huyo, Matilda Tanga, alisema alifahamu binti yake angefanya vizuri kwenye mtihani huo, lakini hakutarajia kuwa angekuwa wa kwanza kitaifa.
“Goldalyn ametuma ujumbe kwa watu wanaowadharau watoto wenye ulemavu wa ngozi, na amethibitisha kwamba mtoto mwenye ualbino akipata upendo na kupewa fursa wanaweza kuufikia uwezo wao,” alisema. Baba mzazi wa Goldalyn, Harrison Tanga, anaikumbuka siku aliyozaliwa mtoto huyo, Aprili 20, 2003.
“Nilipomwona (Goldalyn) nilimkumbatia mke wangu, Goldalyn ni dhahabu yangu,” alisema Tanga. Wakati wa sherehe ya kumpongeza iliyoandaliwa na Jumuiya ya Wenye Ualbino nchini Kenya, Goldalyn alisema alichofanyiwa ni ujumbe kwa jamii kusheherekea ualbino na watu wenye ulemavu huo.
“Tunaweza kuwa vyovyote tunavyotaka,” alisema msichana huyo kwenye sherehe hiyo katika ofisi za ASK, Nairobi. Alitoa mwito kwa wanafunzi wenye ualbino kusoma kwa bidii. “Huwezi kutimiza ndoto zako bila PhD: sala, juhudi na nidhamu,” alisema mtoto huyo.
Kwa mujibu wa Goldalyn, siku za nyuma alikuwa akikaa ndani tu ili watu wasimwone, lakini akapata hali ya kujiamini na kwamba kwa sasa hajisikii vibaya kuwa na ulemavu wa ngozi. Waziri wa Elimu, Dk. Fred Matiang’i alitangaza matokeo siku 19 tu baada ya kumalizika kwa mtihani huo, uliofanywa kuanzia Oktoba 31 mwaka huu.
Kwa mujibu wa Baraza la Taifa la Mitihani Kenya (KNEC), matokeo yamewahi kutolewa kwa sababu mchakato wa kusahihisha, uliharakishwa kwa kutumia mashine ziitwazo automated Optical Mark Recognition Katika matokeo hayo, wanafunzi 9,846 walifanikiwa kupata zaidi ya maksi 400.
Matiang’i alisema, watahiniwa wote kutoka shule za serikali na binafsi, waliopata zaidi ya maksi 400 watapelekwa kusoma kwenye shule za sekondari za serikali. Wanafunzi sita kutoka shule zenye mahitaji maalumu, wamekuwa miongoni mwa watahiniwa 100 bora. Watahiniwa 2,360 walipata maksi chini ya 100.
Mchakato wa kuchagua watakaojiunga na kidato cha kwanza, unatarajiwa kuanza Desemba nne na kazi ya kuwapangia shule itakuwa imekamilika ifikapo Desemba 12. Matiang’i alifurahishwa na matokeo ya shule za serikali. Alisema mwanafunzi wa pili kwa ubora kitaifa, ametoka shule ya serikali ya bweni, Kathigiri na amepata maksi 447.
Alisema, mwanafunzi bora kutoka shule za wenye mahitaji maalumu amepata maksi 426. Kwa ujumla, watahiniwa sita kutoka shule hizo wamepata maksi zaidi ya 400. Kwa mujibu wa Matiang’i watahiniwa kwenye mtihani huo, hawakufanya vizuri kwenye sayansi na masomo maalum.
Rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimuagiza Waziri wa Elimu wa nchi hiyo, Dk Fred Matiang’i wanafunzi ambao hakuwafanya mtihani KCPE kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ya kufiwa, ugonjwa au kujifungua, wapewe wafanye.
Alitoa agizo hilo alipozungumza na Matiang’i kwenye ofisi za Kenyatta katika jengo la Harambee kabla ya kutolewa kwa matokeo ya mtihani huo Msemaji wa Ikulu ya Kenya, Manoah Esipisu, alisema, katika mazungumzo ya Rais Kenyatta na Dk Matiang’i, kiongozi huyo wa nchi alisema, wanafunzi ambao hawakufanya mtihani huo kwa sababu zenye mantiki wakiwemo waliokuwa wamefiwa na wazazi, waliojifungua na waliokuwa wagonjwa, wapewe mtihani na kwamba, utaratibu kama huo unafanyika sehemu nyingi duniani.