Wakati uchaguzi wa udiwani ukitarajiwa kufanyika kesho katika kata 43 nchini, Jeshi la Polisi limesema halitamvumilia yeyote atakayeleta vurugu.
Kauli hiyo imetolewa wakati baadhi ya wanasiasa wakitoa madai ya kuwapo mikakati iliyoandaliwa kuhujumu uchaguzi huo, huku ofisi ya ofisa mtendaji wa Kata ya Saranga jijini Dar es Salaam ikiwa imechomwa moto.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari jana alisema kuna mambo yameanza kujitokeza ya uvunjifu wa amani ikiwemo kuunguzwa ofisi ya mtendaji wa kata hiyo iliyopo wilayani Ubungo na watu kupigana wakiwa kwenye kampeni mkoani Mwanza.
IGP Sirro alisema jeshi hilo litahakikisha wale wote waliofanya matukio hayo wanachukuliwa hatua za kisheria.
Aliwataka wanasiasa kufanya siasa na si kufanya fujo na kwamba, yeyote atakayepatikana amevunja sheria ya nchi atashughulikiwa kama wahalifu wengine.
“Ninawaomba wananchi mchague madiwani walio sahihi msichague wale ambao wanatarajia kuleta vurugu kwa kuwa watashughulikiwa na tunaendelea na upelelezi ili kuwabaini wote waliohusika kuunguza ofisi ya ofisa mtendaji wa kata,” alisema IGP Sirro.
Licha ya kuungua kwa ofisi hiyo usiku wa kuamkia jana, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema uchaguzi utaendelea kama ulivyopangwa. Tume imesema vifaa vingi vya uchaguzi vimeteketea.
Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi (NEC) Hamis Mkunga alisema jana katika taarifa kwa umma kuwa tayari ofisi yake imekwishafanya utaratibu mwingine ili kuhakikisha vifaa vyote vya uchaguzi vilivyoteketea vinapatikana.
Mkunga alisema chanzo cha moto huo ni hujuma kwa kuwa walioshuhudia walipofika eneo la tukio walikuta dumu la mafuta ya petroli na kwamba vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi.
Alisema vyombo vya usalama wilayani Ubungo vimejulishwa na kuwahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa usalama utaimarishwa na kuwataka wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.
Mkuu wa Idara ya Uchaguzi NEC, Irene Kadushi alisema Kata ya Saranga ina vituo vya kupigia kura 139.
Alisema utunzaji wa vifaa vya uchaguzi zimehamishiwa katika Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa usalama zaidi.
Mikoa inayotarajiwa kufanyika uchaguzi ni Geita, Mwanza, Dodoma, Ruvuma, Tabora, Songwe, Mbeya, Rukwa, Lindi, Mtwara, Iringa, Singida, Simiyu, Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Manyara na Morogoro.
Malalamiko Chadema
Chadema katika mikoa ya Arusha na Iringa imesema imeandika barua kwa NEC na makao makuu ya polisi kueleza kuhusu kukiukwa utaratibu wa uchaguzi na kuwepo njama za kufanywa vurugu katika uchaguzi huo.
Wakizungumza na waandishi wa habari, mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema; Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro na Kaimu Katibu wa Chadema mkoani hapa, Elias Mungure walisema wanaomba NEC na vyombo vya dola kuingilia kati ili uchaguzi uwe huru na haki.
Lema alisema tangu kuanza kampeni za uchaguzi mdogo, viongozi wa Chadema wamekuwa wakivamiwa na hakuna hatua zinazochukuliwa na kwamba kuna taarifa za njama za wengine kuvamiwa ili kuvuruga uchaguzi.
Meya Lazaro alisema wameshangazwa na viongozi wa Serikali kwenda kwenye kampeni na kutoa ahadi kitu ambacho ni kinyume cha sheria za uchaguzi.
Mungure alisema wameandika barua NEC na kwa vyombo vya juu vya Serikali kuhusu hujuma na ukiukwaji wa utaratibu unaofanyika.
Hata hivyo, Kamaanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana kuwa hana taarifa za mipango ya vurugu na akawataka wenye taarifa kuzipeleka polisi.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa akizungumza na waandishi wa habari jana ameitaka polisi kuwaacha wananchi wachague mgombea wanayemtaka akidai kuna hujuma zinafanyika na taarifa ameshazifikisha kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) .
Pia, ametaka watendaji wa Serikali waache kuingilia masuala ya siasa bali watekeleze majukumu yao, huku akitaka mkurugenzi wa Halmashauri ya Iringa kusimamia uchaguzi wa Novemba 26,2017 kwa haki.
Mratibu mwandamizi wa uchaguzi Kata ya Kitwiru wa Chadema, Edward Kinabo amedai kuna njama za kuvuruga uchaguzi usiwe wa amani, uhuru na haki.
Kinabo amesema wameonana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi na kumweleza kuhusu njama hizo anazodai zinafanywa na polisi na CCM.
Amesema wanachama saba wa Chadema wako polisi kwa wiki moja sasa bila kufikishwa mahakamani jambo ambalo ni kinyume cha sheria.
Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe amewahakikishia wananchi watachagua kiongozi wanayemtaka na si kwa kulazimishwa kwa kutishwa.
Imeandikwa na Pamela Chilongola, Mussa Juma na Berdina Majinge.
Mwananchi
Mwananchi