Meya wa Manispaa ya Songea, Alhaji Abdul Shaweji ameelezea yaliyojiri kabla ya kifo cha mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama.
Akizungumza na gazeti hili jana, Shaweji alisema Novemba 22 wakati Gama akianza safari ya kutokea Dodoma kwenda Songea kwa ajili ya kushiriki ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa walikuwa wakiwasiliana kila wakati.
“Kila sehemu aliyofika alinipigia simu. Nakumbuka alipofika Iringa alinipigia na kutanitaarifu yupo njiani kuja Songea kwa ajili ya shughuli za jimbo na kumpokea Waziri Mkuu. Alifika Songea saa nne usiku akiwa mchangamfu na kuzungumza na mkewe nyumbani kwake katika Kijiji cha Likuyu Fusi.
Alisema ilipofika saa sita usiku alimwambia mkewe mama Muyanga kwamba anakwenda msalani, wakati anarudi ghafla aliishiwa nguvu ndipo mkewe alimwita dereva wake ambaye wanaishi naye katika nyumba yao na kuanza safari za kumpeleka Gama katika Hospitali ya Peramiho kwa ajili ya matibabu.
Shaweji alisema Gama alisindikizwa Peramiho na watu wasiozidi 10 na alifariki dunia saa sita usiku wa kuamkia jana katika hospitali hiyo wakati akipatiwa matibabu.
Wakati mbunge huyo akifariki dunia, alisema mkewe mama Muyanga na watoto wake wawili walikuwepo.
“Kifo cha Gama kilisababisha mama Muyunga kupata presha na kulazwa hospitalini hapo takriban kwa saa mbili kuanzia saa sita hadi saa nane usiku,” alisema Shaweji.
Kutokana na msiba huo wa Gama ambaye kabla ya kupata ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Spika wa Bunge, Job Ndugai katika taarifa alisema wamesikitishwa na kifo cha mbunge huyo.
“Kabla ya kifo chake alirejea Novemba 11 mwaka huu akitokea India alikokuwa akipatiwa matibabu. Novemba 21 alitokea Dar es Salaam kurejea Songea kwa kupitia Dodoma ili kushiriki mapokezi ya ziara ya Waziri Mkuu iliyoanza Novemba 23,” alisema Ndugai katika taarifa ya Bunge.
Taarifa hiyo ilieleza Novemba 22 saa sita usiku aliugua ghafla na baada ya ofisi ya Bunge kupata taarifa iliandaa ndege maalumu kwa ajili ya kumsafirisha kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi. Hata hivyo, madaktari wa Peramiho walishauri asisafirishwe hadi hali yake itakapotengamaa.
Bunge katika taarifa ilisema Gama atazikwa keshokutwa katika Kijiji cha Likuyu Fusi, Manispaa ya Songea.
Akizungumza gazeti hili, Issa Fussi ambaye ni msemaji wa familia na mdogo wa Gama alisema alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu.
Fussi alisema msiba huo ni pigo kwa familia kwa kuwa Gama alikuwa nguzo akitegemewa katika masuala mbalimbali ya maendeleo na kifamilia.
Wakati huohuo, Rais John Magufuli amemtumia rambirambi kwa Spika Ndugai kutokana na kifo cha Gama.
Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu jana Rais Magufuli alisema, “Nakupa pole Spika Ndugai, wabunge na wafanyakazi wa ofisi yako; na kupitia kwako naomba ufikishe salamu zangu za pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa jimbo la Songea Mjini na mkoa wa Ruvuma, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu.”
Pia ametoa pole kwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho na wana CCM kwa kumpoteza kada aliyekiwakilisha vyema chama hicho kwa nafasi yake ya ubunge.
Rais Magufuli alisema Gama aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo ukuu wa wilaya, mkoa na ubunge alikuwa kiongozi hodari, aliyefanya kazi kwa kujiamini na aliyependa kupigania masilahi ya wananchi bila kuchoka.
Mwananchi
Mwananchi