Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amewekwa kizuizini na Jeshi la Ulinzi usiku wa kuamkia jana katika mji mkuu wa Harare, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amethibitisha.
Zuma alisema jana kwamba alipigiwa simu na Mugabe mwenyewe. Taarifa kutoka ofisi ya Zuma ilisema: "Rais Zuma alizungumza na Rais Robert Mugabe mapema leo na amedokeza kwamba anazuiliwa nyumbani kwake lakini alisema yuko salama."
Kuanzia Jumanne wanajeshi walionekana wakivinjari na kupiga doria katikati ya Harare, baada ya kuteka kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji la Zimbabwe (ZBC) kwa kile kilichoelezwa wanawalenga “wahalifu”.
Hatua hiyo ya jeshi inaweza kuwa ni mpango wa kumwondoa Mugabe na kumweka katika nafasi hiyo makamu wake aliyefukuzwa kazi wiki iliyopita Emmerson Mnangagwa, shirika la BBC limeripoti.
Ofisa mmoja wa jeshi, Meja Jenerali Sibusiso Moyo alionekana kwenye televisheni baada ya kukiteka kituo hicho akisema Mugabe na familia yake wako “salama na afya njema na ulinzi wao ni wa uhakika ".
Meja Jenerali Moyo alisema, “Sisi tunawatafuta wahalifu waliomzunguka yeye (Mugabe) ambao wanafanya uhalifu na kusababisha machungu ya kijamii na kiuchumi nchini.”
"Mara tutakapokuwa tumekamilisha operesheni hii, tunatarajia kwamba hali itarudi kuwa ya kawaida."
Kufukuzwa kazi kwa Mnangagwa wiki iliyopita kutengeneza njia kwa mke wa Rais Mugabe, Grace kuteuliwa katika nafasi hiyo hivyo kuwa na matumaini ya kuteuliwa kuwa mrithi wa kiti cha mumewe.
Milio mizito ya bunduki ilisikika kaskazini mwa mji wa Harare hadi jana alfajiri.
Social Plugin