Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Hebron Mwakagenda amesema wameazimia kufungua kesi ya kudai haki ya kufanya maandamano ya amani nchini baada ya maandamano yao yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Oktoba 30, mwaka huu kuzuiliwa na Jeshi la Polisi.
Mwakagenda amesema Oktoba 7, mwaka huu walitoa tamko kwa umma la kukusudia kufanya maandamano ya amani nchi nzima kumpongeza na kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kusimamia rasilimali za taifa pamoja na kupiga vita rushwa lakini Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam liliwazuia.
Pia maandamano hayo yalilenga kufikisha ujumbe kuhusu haja ya serikali kurejesha mchakato wa katiba mpya ili taifa liweze kupata katiba mpya chini ya uongozi wa Rais Magufuli lakini jitihada zao ziligonga mwamba.
“Kwa uzito huu JUKATA tulimwandikia Rais Magufuli ili ayapokee maandamano hayo ambayo yalikuwa yamepangwa kuanzia ofisi zetu zilizopo Mwenge hadi Viwanja vya Mnazi Mmoja, hadi leo hatujapata majibu ya barua iliyotumwa Ikulu kwa Rais Magufuli juu ya ombi letu. Lakini tulipokea barua kutoka Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ikikataza kufanyika kwa maandamano hayo ya c amani,” amesema Mwakagenda.
Jeshi la Polisi lilizuia maandamano hayo kwa sababu tatu, zikiwemo kwamba Rais Magufuli hakuthibitisha kushiriki kwenye maandamano hayo, kufanya maandamano umbali mrefu kutoka Mwenge hadi Mnazi Mmoja kutaathiri shughuli kwa kufunga barabara na Oktoba 30 ndiyo siku ambayo mitihani ya kidato cha nne ingekuwa ikifanyika.
“Kwa sababu hizi zilizotumika kukataza maandamano, tumefikia maamuzi ya kwenda kufungua kesi mahakamani kudai haki ambayo inaminywa na kukandamizwa na Jeshi la Polisi kwa kutumia sababu nyepesi.
“Tupo kwenye hatua za mwisho kutekeleza uamuzi huu na kwamba jopo la mawakili wasomi wasiopungua kumi wakiongozwa na Dkt. Rugemeleza Nshala watahusika katika mchakato huu wa kudai mahakamani haki hii ya kufanya maandamano ya amani,” alifafanua.
Mwakagenda alihitimisha kwa kusema Tanzania inafuata misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria ambapo misingi mikuu ya kidemokrasia ni pamoja na uhuru wa watu kukusanyika na kujadiliana kwa mujibu wa sheria kujadili masuala yanayohusu taifa.
Social Plugin