Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Audio : KAMPENI MENEJA WA KATAMBI,MWENYEKITI WA BAVICHA SHINYANGA MJINI AANIKA SIRI ZA KATAMBI KUHAMIA CCM..MSIKILIZE HAPA


Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema wilaya ya Shinyanga Mjini Samson Ng’wagi amefichua siri ya harakati za aliyekuwa Mwenyekiti wa BAVICHA taifa Patrobas Katambi aliyejiondoa CHADEMA na kuhamia CCM mapema wiki hii huku akiwaomba viongozi wa CHADEMA taifa wasishughulike na Katambi wamwachie yeye kuwa ni saizi yake.

Ng’wagi ambaye alikuwa Kampeni Meneja wa Patrobas Katambi wakati akigombea ubunge jimbo la Shinyanga Mjini katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,amesema kuhama kwa Katambi kunatokana na hasira ya kukosa uteuzi wa kugombea ubunge wa Afrika Mashariki ndani ya CHADEMA.

Akizungumza leo Alhamis Novemba 23,2017 katika kikao na waandishi wa habari kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa baraza la vijana wilaya ya Shinyanga Mjini katika ukumbi wa ofisi za Chadema Kanda ya Serengeti zilizopo mjini Shinyanga,Ng’wagi alisema hana jipya kwani harakati zake hazikuanza jana wala juzi ni suala la siku nyingi.



“Harakati za kuondoka Chadema zilikolea hasa alipokosa uteuzi wa kugombea ubunge Afrika wa Afrika Mashariki ndani ya chama,alinung’unika sana,kwa kuwa ni rafiki yangu wa karibu niliongea naye na kama haitoshi nilifika nyumbani kwao na kuzungumza na mama yake ambaye pia alieleza masikitiko yao kwanini mwanaye hakuteuliwa kugombea nafasi hiyo”,alieleza Ng’wagi.


“Nilishauriana na mama yake tukamshauri Katambi aendelee kubakia Chadema ingawa baba yake alimtaka aachane na siasa kama haoni maslahi”,alisema.

Ng’wagi alisema hoja za Katambi za ubinafsi,ukabila na ubaguzi ndani ya chama hazina mashiko yoyote isipokuwa alikuwa na ugomvi wa maslahi binafsi na chama na alishindwa kutambua kuwa CHADEMA ina watu wengi sana na wenye sifa,uwezo na weledi wa kugombea nafasi ya ubunge wa Afrika Mashariki.

“Lakini pia siyo kweli kwamba Katambi alitumiwa kama karai ndani ya chama chetu,hakuwa karai alipewa nafasi za juu katika chama,kwani aliaminiwa na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa BAVICHA taifa na kuwa na sifa ya kuingia kwenye vikao vyote vikuu vya kitaifa”,alisema.

“Kama hiyo haitoshi alipewa nafasi ya kugombea ubunge jimbo la Shinyanga Mjini akiwa hana umaarufu wowote ndani ya jimbo na hakuwa na uwezo wa kifedha za kumwezesha kufanya kampeni,hivyo chama kilimpa fedha kwa ajili ya kuendeshea kampeni”,aliongeza.

Alisema kama hiyo haitoshi Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema alitoa gari lake bila malipo kwa ajili ya Katambi kulitumia katika kufanyia kampeni zake huku wanachama na wapenzi mbalimbali wa chama wakijitolea kumchangia kumuwezesha kufanya kampeni zake.

“Katambi alikuwa jimboni miezi miwili tu kabla ya uchaguzi,chama kilimuamini na kumpa nafasi pamoja na changamoto na mpasuko ndani ya chama ngazi ya jimbo alizosababisha yeye akitumia kofia ya uenyekiti wa Bavicha taifa,baadhi ya viongozi na wanachama tulisimama imara kumtakasa na kumuondolea utando na kutu aliyokuwa nayo hasa ya makazi yake ya kudumu”,alifafanua.

Aliongeza kuwa siku moja kabla ya kuhamia CCM.Katambi alimweleza Ng’wagi kuwa kuna haja ya kubadilisha chama kwa sababu ya siasa za sasa hazieleweki.

“Novemba 19 mwaka huu majira ya saa 6 usiku,Katambi alinipigia simu akisema kuna haja ya kubadilisha chama kwa sababu ya siasa za sasa hazieleweki na pia aliahidi kuna shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kuwashawishi ambao alitaka tuhame nao”,aliongeza.

“Nilimshauri kwamba mwenyekiti hilo siyo jambo jema wananchi wana matumaini makubwa na sisi kumbuka kura walizotupa mwaka 2015 ulizidiwa kura 3,000 na tukifanya hivyo tutajiondolea heshima tuliyopewa na wana Shinyanga na taifa kwa ujumla”,alieleza Ng’wagi.

Ng’wagi aliyejinasibu kuwa ni rafiki wa karibu na mashauri wa Katambi alisema baada ya maongezi marefu na kuonesha msimamo wake wa kutokisaliti chama,Katambi alikubali kuwa hatahama na ataendelea kupambana na CCM.

Hata hivyo alisema baraza la vijana Shinyanga mjini ipo imara na kuondoka kwa Patrobas Katambi hakitawaathiri kwa namna yoyote na msimamo wao ni kuendeleza harakati za kudai haki na kuimarisha demokrasi na kuwaenzi waasisi wao akiwemo Bob Makani na Shelembi Magadula.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini,Hamis Ngunila alisema Chadema bado ipo hai na kuwataka wana CHADEMA kuwa makini na watu wanaoingia katika chama na kujinasibu kuwa ni wasomi na wanajua kila kitu.

“Tunamtakia kila la heri huko alikoenda akatumike kama beseni,ameondoka kwenye chama yeye kama Katambi,chama bado kipo hai,aliyekuwa anaiamini CHADEMA atabaki CHADEMA na aliyekuwa anamwamini Katambi basi amfuate Katambi”,aliongeza Ngunila.

MSIKILIZE HAPA SAMSON NG'WAGI AKIMWAGA SIRI ZA KATAMBI NA KAFULILA


Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema wilaya ya Shinyanga Mjini Samson Ng’wagi akitoa tamko la BAVICHA wilaya ya Shinyanga Mjini leo-Picha na Kadama Malunde- Malunde1 blog
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema wilaya ya Shinyanga Mjini Samson Ng’wagi akionesha nyaraka alizoachiwa na Patrobas Katambi
Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Shinyanga Mjini,Hamis Ngunila akizungumza katika kikao hicho
Katibu wa Chadema kata ya Lubaga Nyamusi Marera ambaye alikuwa Wakala mkuu wa Katambi wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015
Viongozi wa Chadema kutoka maeneo mbalimbali wilaya ya Shinyanga Mjini.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com