Aliyekuwa Mwenyekiti wa baraza la Vijana Chadema taifa (BAVICHA),Patrobas Katambi amehamia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema kuwa alisema kama ataitwa msaliti basi atakuwa kundi la wasaliti wa nchi ya Tanzania.
Katambi ametangaza kujiondoa Chadema leo Jumanne Novemba 21,2017 katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kinaoendeshwa na mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt. John Pombe Magufuli jijini Dar es salaam.
Akizungumza katika kikao hicho, Katambi alisema mambo mengi katika nchi yalikuwa yanaenda mrama na sasa yamebadilika hivyo ameamua kujiunga CCM ili kujenga chama hicho.
“Mambo mengi yalikuwa mrama na watu tunapenda mabadiliko ila hatutaki kubadilika, kama nitaitwa msaliti basi nitakuwa msaliti kundi la wasaliti wa nchi hii, ukombozi ulishapatikana, siyo tunachokisema majukwaani ndiyo tunachokiishi",alisema Katambi.
"Maisha tunayoyahubiri siyo tunayoishi, ukienda jimboni kwake, vijana kama nguvu kazi ya taifa, tunajadili ‘personalities’ badala ya ‘issues’ mawazo mbadala,niwaombe nijiunge na CCM siyo kwa sababu za madaraka ila tuijenge, CCM inatoa nafasi kwa vijana, vijana kwa upinzani ni sawa na karai katika ujenzi”,aliongeza Katambi.
Mbali na Katambi kujiunga CCM, Katibu mkuu wa Wizara ya Maji, Profesa Kitila Mkumbo ambaye alikuwa kada wa ACT,naye ametangazwa rasmi kujiunga na CCM mbele ya kikao hicho.
Wengine waliotangazwa kujiunga na CCM ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani, Lawrence Masha na waliokuwa wanachama wa ACT; Samson Mwigamba na Albert Msando.