KATEKISTA AFARIKI BAADA YA KUENDESHA IBADA YA MAZISHI MAKABURINI KATAVI


Mwalimu wa dini wa Kanisa Katoliki (katekista) Jimbo la Mpanda,mkoani Katavi Noel Sitemele amefariki dunia muda mfupi baada ya kumaliza kuongoza ibada ya mazishi ya muumini wake yaliyofanyika katika makaburi ya Mchakamchaka Kijiji cha Majalila wilayani Tanganyika mkoani Katavi.

Katekista huyo alikuwa akitoa huduma ya kiroho katika Kigango cha Mchakamchaka kilichopo katika Parokia ya Mpanda Ndogo katika Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi. 

Akizungumzia mkasa huyo, Diwani wa Kata ya Mpanda Ndogo, Hamad Mapengo alisema licha ya Sitemele kuwa mwalimu wa dini, katika uhai wake alikuwa pia Mwenyekiti wa Kijiji cha Majalila kilichopo katika Halmashauri ya Mpanda wilayani Tanganyika.

Mapengo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mpanda, alisema Katekista alifariki dunia juzi saa 11 jioni muda mfupi baada ya kufikishwa zahanati ya kijiji Majalila kutibiwa.

Alisema kabla ya kukutwa na umauti, Katekista huyo alikuwa mwenye siha njema na aliongoza ibada ya mazishi ya muumini wake hadi mwisho katika makaburi ya Kigango cha Mchakamchaka kilichopo katika Kijiji cha Majalila ambapo alianza kujisikia vibaya.

“Baada ya kumaliza ibada hiyo ya mazishi, alianza kujisikia vibaya hivyo akalazimika kurejea nyumbani kwake na kuwaacha waombolezaji makaburini,” alieleza Mpaengo.

 Alisema, baada kufika nyumbani kwake, hali yake iliendelea kuwa mbaya na aliomba msaada kutoka kwa majirani zake wamkimbize kwenye kituo cha afya kwa matibabu.

Inaelezwa zahanati hiyo haiko mbali kutoka alikokuwa akiishi mwalimu huyo wa dini. 

Mwenyekiti alisema, taarifa za kifo cha Katekista huyo zilizagaa haraka kijijini humo na kuwafikia waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu aliyeongozewa ibada ya mazishi na Katekista huyo waliopata simanzi kubwa wengine wakiwa hawaamini jambo hilo.

Maziko yake yalifanyika jana makaburi ya kigango cha Mchakamchaka Kijiji cha Majalila. Padri Paschal Kipenye wa Parokia ya Mpanda Ndogo aliongoza ibada ya mazishi yaliyohudhuriwa na mamia ya waombolezaji akiwemo Mbunge wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso.

IMEANDIKWA NA PETI SIYAME - HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post