Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemuachia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kupokea rushwa ya Sh 323 milioni toka kwa James Rugemalira fedha ambazo ni sehemu ya zilizotoka kwenye Akaunti ya Tegeta Esrow.
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa amemuachia huru Rugonzibwa leo Alhamisi baada ya Mwendesha Mashtaka Mwandamizi wa Takukuru, Leonard Swai kuomba kesi hiyo iondolewe mahakamani hapo chini ya kifungu cha 98 (a) cha Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA) na Mahakama kuridhia.
Rugonzibwa alifikishwa na Takukuru mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 14, 2015 akikabiliwa na shtaka la kupokea rushwa ya Sh 323 milioni toka kwa Rugemalira fedha ambazo ni sehemu ya zile Akaunti ya Tegeta Esrow.
Hata hivyo baadaye alibadilishiwa hati ya Mashtaka na kusomewa upya ambayo hayakuonyesha tena kuwa fedha zilizopokelewa na Mujunangoma toka kwa Rugemalira ni sehemu ya fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kupitia hati hiyo mpya, Rugonzibwa alikuwa akidaiwa kuwa Februari 5, 2014 akiwa mtumishi wa Serikali kama Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alipokea rushwa ya Sh Sh323 milioni kupitia akaunti yake namba 00120102602001 iliyopo kwenye Benki ya Mkombozi .
Alidaiwa kuwa alipokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Rugemalira, ambaye ni mshauri huru wa kitaalamu, mkurugenzi wa VIP na mkurugenzi wa zamani wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL kama tuzo kwa kushughulikia mambo ya ufilisi wa muda wa kampuni hiyo.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, alikana na upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa umekwisha kamilika.