KUTOKA MBEYA MPAKA KUJA KUWA RAIS ZIMBABWE

Mwaka 1962 mji wa Mbeya ulikuwa mwenyeji wa kijana mmoja mwenye umri wa miaka 20 tu aliyeungana na wenzake wa chama cha Zimbabwe African People’s Union (Zapu) akitokea Zambia.

Hakukaa muda mrefu akapelekwa Misri kisha China lakini aliporejea Zimbabwe kukabiliana na wakoloni alikamatwa akafungwa miaka 10 na alipotoka jela hakuacha harakati zake hadi Zimbabwe ilipopata uhuru.

Anafahamika kwa jina la utani la Mamba kutokana na kundi aliloasisi Dar es Salaam, lakini majina yake ni Emmerson Dambudzo Mnangagwa (75), ambaye jana dunia ilimshuhudia akila kiapo kwenye uwanja wa michezo baada ya kutawazwa kuwa Rais wa Zimbabwe.

Anakuwa rais wa pili katika historia ya Zimbabwe akimrithi mkongwe Robert Gabriel Mugabe aliyejiuzulu Novemba 21. Mamba, kama lilivyo jina la utani, ni askari wa kweli na mpambanaji.

Kujiuzulu kwa Mugabe kulisababisha shangwe; nderemo na vifijo kwa Wazimbabwe walioko ndani na nje ya Zimbabwe. Kadhalika shangwe zilitawala baada ya Mnangagwa kuapishwa rasmi siku mbili tu tangu aliporejea kutoka Afrika Kusini alikokimbilia akihofia maisha yake baada ya kufukuzwa na Mugabe Novemba 6.

Mugabe hakujiuzulu kwa hiari bali ni baada ya maandamano ya wananchi chini ya usimamizi wa jeshi. Novemba 19 chama cha Zanu PF kilimwondoa Mugabe katika nafasi ya uongozi na kikamtangaza Mnangagwa aliyekuwa uhamishoni kuwa rais; pili, kilimpa Mugabe muda hadi Novemba 20 mchana ajiuzulu urais wa Zimbabwe.

Novemba 21, muda mfupi baada ya Bunge kuanza kujadili hoja ya kumwondoa, Mugabe mwenye umri wa miaka 93 aliwasilisha barua kwa Spika wa Bunge akitangaza kuachia madaraka. Hatua hiyo ndiyo iliyomwezesha Mnangagwa kurejea nchini.

Uanaharakati
Mnangagwa alizaliwa Septemba 15, 1942 huko Shabani, kusini mwa Zimbabwe ukoo wa Karanga kutoka kabila kubwa la Shona. Mwaka 1955 wazazi wake wakulima waliolazimika kukimbilia Zambia kwa sababu ya upinzani wao dhidi ya walowezi.

Huko alisoma darasa la V na VI katika Shule ya Bweni ya Mumbwa kuanzia 1956 hadi 1957. Mwaka 1960 alifukuzwa Chuo cha Ufundi cha Hodgson kwa kosa la kujihusisha na siasa; vurugu ziliibuka. Alikuwa amejiunga na tawi la wanafunzi wa United National Independence Party (UNIP) lililokuwa likiendesha harakati na akawa mmoja wa viongozi.

Mnangagwa aliamua kuanzisha kampuni ya ujenzi ya Nampala ambayo ilidumu miezi mitatu tu. Katika kipindi hicho aliombwa kujiunga na UNIP ili asaidie kuhamasisha na kuanzisha tawi katika mji wa Chililabombwe kazi aliyoifanya hadi mwishoni mwa 1961. Akarejeshwa Lusaka ambako alikuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa UNIP.

Mwaka 1962 alivutiwa na harakati za Zimbabwe akajiunga na chama cha Zapu. Alipelekwa Tanzania ambako aliishi kambi ya mafunzo Mbeya na watu wengine kama James Chikerema, Clement Muchachi na Danha. Aprili 1963, yeye na makada wengine 12 wa Zpu walipelekwa Dar es Salaam na baadaye wakasafirishwa kwenda chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Heliopolis, Misri.

Agosti 1963, yeye na wenzake 10 kati ya makada 13 waliokuwa wanachukua mafunzo ya kijeshi Misri waliamua kujiunga na chama kipya kilichoanzishwa cha Zimbabwe African National Union (Zanu).

Serikali ya Misri ambayo ilikuwa inaitambua Zapu iliyokuwa na fedha na siyo Zanu hohehahe iliwaweka ndani. Mugabe aliyekuwa Tanzania alijulishwa mkasa wa vijana hao.

Alimtuma Trynos Makombe kwenda Misri kuomba vijana hao waachiwe na alipofanikiwa walirejea Dar es Salaam.

Halafu vijana sita kati yao walikwenda Zimbabwe ilhali Mnangagwa na wenzake watano walijiunga na kambi ya chama cha Frelimo, Bagamoyo Agosti 1963. Mnangagwa alipelekwa China na tawi la Zimbabwe African National Liberation Army (ZANLA) ambako alikaa miezi miwili Chuo Kikuu cha Peking.

Miezi mitatu akasomea upiganaji Nanking halafu alisomea uhandisi wa kijeshi pamoja na Felix Santana, Robert Garachani, Lloyd Gundu, Phebion Shonhiwa na John Chigaba.

Mei 1964 alikwenda Tanzania ambako waliasisi kundi waliloliita Mamba.

Baadaye walikwenda kuhudhuria mkutano mkuu wa uchaguzi wa Zanu uliofanyika Mkoba, Gweru na walifika siku moja kabla ya mkutano huo. Matokeo ya uchaguzi yakawa Mchungaji Ndabaningi Sithole akachaguliwa kuwa rais wa chama, makamu wake alikuwa Leopold Takawira; Herbert Chitepo akawa mwenyekiti na Mugabe akawa katibu mkuu.

Baada ya mkutano mkuu wenzake watatu walikamatwa kwa madai ya kuingiza silaha. Januari 1965, Mnangagwa alikamatwa baada ya kusalitiwa na mmoja wao kuwa Mamba ndio walihujumu reli na treni ya Masvingo.

Baada ya mateso makali Mnangagwa alikiri na chini ya sheria ya usalama wa taifa ya mwaka 1960 alikuwa ahukumiwe kifo. Mawakili wake walijitahidi kujenga hoja kwamba alikuwa chini ya umri wa miaka 21, hivyo hawezi kunyongwa ndipo alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela. Mwaka wa kwanza alitumikia katika gereza la Harare na kisha akapelekwa gereza la Mtaa wa Grey na baadaye gereza la Khami yote yako Bulawayo.

Hata baada ya kumaliza kifungo chake bado aliendelea kushikiliwa katika gereza la Khami kisha Harare na wapigania uhuru wengine kama Mugabe, Enos Nkala, Maurice Nyagumbo, Edgar Tekere na Didymus Mutasa. Baadaye alisafirishwa hadi Zambia walikokuwa wazazi wake.

Wakatui wengi wakifungwa hutoka wakiwa na ujuzi wa ufundi seremala Mnangagwa alitumia muda wake kusoma hadi kuhitimu shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Zambia kwa njia ya posta.

Baadaye alikwenda Msumbiji kushiriki vita vya ukombozi dhidi ya mkoloni Ureno. Huko alikutana tena na Mugabe na akawa msaidizi wake na mlinzi wake. Katika mkutano mkuu wa Chimoio mwaka 1977 alichaguliwa kuwa Msaidizi Maalumu wa Rais na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Zanu.

Mnangagwa na Mugabe ndio waliokwenda Uingereza kufanya mazungumzo yaliyowezesha kutiwa saini makubaliano ya Lancaster ya kuitambua Jamhuri ya Zimbabwe. Hatimaye mwaka 1980 Zimbabwe ilipata uhuru.

Baada ya uhuru
Baada ya uhuru alikuwa Waziri wa Usalama wa Taifa. Baadaye akawa mwenyekiti wa mazungumzo yaliyowezesha ushirikishwaji wa majeshi ya ZANLA, Zimbabwe People’s Revolutionary Army (ZIPRA) na Rhodesian Army.

Katika kipindi hicho alikuwa mpelelezi mkuu aliyesimamia Shirika la Upelelezi. Yalipoibuka mapigano dhidi ya majeshi ya chama cha Zapu kilichokuwa kinaongozwa na Joshua Nkomo inadaiwa alisimamia ukandamizwaji mkubwa na kuuawa kwa watu wengi wa kabila la Ndebele, Matabeleland.

Mnangagwa amekuwa akikanusha kuhusika. Japokuwa mgogoro uliisha na Zapu ya Nkomo ikaunganishwa na Zanu ya Mugabe kuunda Zanu PF, bado analaumiwa kwa mauaji hayo.

Nafasi nyingine ambazo amewahi kushika Mnangagwa ni Waziri wa Haki, Sheria na Masuala ya Bunge na kiongozi wa waliowengi. Kwa miezi 15 alikuwa Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje kati ya 1995 na 1996.

Kampeni za urais
Mwaka 2014 alipoteuliwa kuwa Makamu wa Rais, alianza kufikiriwa kuwa mrithi sahihi wa Mugabe akistaafu au akifariki dunia. Mwaka 2016 akaanzisha kundi aliloliita Lacoste kwa ajili ya kumfanyia kampeni za yeye kuwa rais.

Lacoste lilipambana na kundi la G40 lililokuwa linafadhiliwa na Grace Mugabe, mke wa Rais Mugabe ambaye pia alikuwa anataka urais. Grace ndiye kiini cha kufukuzwa Mnangagwa ili yeye asiwe na mpinzani lakini Grace amekuwa kiini cha Mugabe kujiuzulu.

Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post