MALIMA AFUTIWA KESI.....SIKU SITA TU BAADA YA KUTEULIWA KUWA MKUU WA MKOA WA MARA

Siku sita baada ya Adam Malima kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mahakama imemfutia kesi ya shambulio iliyokuwa ikimkabili.

Rais John Magufuli, Alhamisi Oktoba 26,2017 alifanya uteuzi mbalimbali ukiwemo wa wakuu wa mikoa.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatano Novemba 1,2017 imeifuta kesi dhidi ya Malima na mwenzake.

Malima ambaye amesharipoti mkoani Mara hakuwepo mahakamani wakati uamuzi huo ukitolewa.

Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage ameifuta kesi hiyo na kuwaachia huru washtakiwa baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa kuomba ifutwe.

Chini ya kifungu cha 91 (1) cha Mwenendo wa Mashauri ya Jinai, Mutalemwa ameomba shauri lifutwe kwa sababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) hana nia ya kuendeleza mashtaka dhidi ya washtakiwa.

Baada ya ombi hilo kuwasilishwa, Hakimu Mwijage alimuhoji Mutalemwa iwapo kuna sababu ya kuifuta kesi hiyo na kama hana hataifuta.

Wakili Mutalemwa alisoma kifungu hicho akisema kinampa mamlaka DPP kuiondoa kesi mahakamani wakati wowote anapoona inafaa na pia, kinamruhusu kuirudisha mahakamani.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mwijage alikubali kuwaachia huru washtakiwa.

Shauri hilo lilikuwa katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Waliposomewa maelezo ya awali, Malima na mshtakiwa mwenzake Ramadhani Kigwande walikubali maelezo yao binafsi, siku ya tukio walikuwepo Masaki, walikamatwa na kushtakiwa.

Walikana maelezo mengine kuhusu mashtaka yanayowakabili.

Katika kesi hiyo, Malima aliyewahi kuwa naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne na mbunge wa zamani wa Mkuranga alidaiwa Mei 15,2017 katika eneo la Masaki kwa makusudi alimzuia ofisa wa polisi Konstebo Abdu kufanya kazi yake halali.

Malima alidaiwa kumzuia askari huyo kumkamata Ramadhani Kigwande kwa kosa la kumshambulia Mwita Joseph.

Kigwande alidaiwa Mei 15,2017 eneo la Masaki wilayani Kinondoni akiwa na nia ya kumzuia Mwita Joseph, ambaye ni ofisa operesheni wa kampuni ya Priscane Business Enterprises alipokuwa akimkamata kwa kupaki vibaya gari alimshambulia na kumsababishia maumivu.

Waliposomewa mashtaka, washtakiwa walikana na walikuwa nje kwa dhamana  kwa kila mmoja kuwa na mdhamini mmoja ambaye alisaini bondi ya Sh5 milioni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post