MBOWE ATOA TATHIMINI KAMPENI ZA UDIWANI

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema wamewazidi CCM kimkakati katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika kesho katika kata 43 nchini.

Mbowe amesema chama tawala hakina mpango mkakati wa kufahamu mambo gani wananchi wanataka na shida gani zinawakabili zaidi ya kuzungumzia kwa jumla na kujinasibu kufanya mambo makubwa ikiwamo kujenga barabara, kununua ndege na kupambana na mafisadi.

Amesema leo Jumamosi Novemba 25,2017 kuwa ndiyo maana katika kampeni za kuwanadi wagombea wa uchaguzi huo alinadi ajenda tatu ambazo ni dhana ya uhuru, maendeleo na demokrasia.

Mbowe amesema maendeleo hayapimwi kwa kununua magari, kujenga viwanja vya ndege, kupambana na mafisadi bali yanapimwa kwa maisha ya mwananchi mmoja mmoja.

"Tunaaminishwa uchumi unakuwa kwa sababu nchi imenunua ndege, inapambana na mafisadi na inajenga viwanja vya ndege, hayo ni mambo mazuri hakuna anayepinga, lakini je, mwananchi wa kawaida ananufaika vipi," amesema Mbowe.

Amesema hali ya maisha ni ngumu, hivyo Serikali isijifungie na isizibe masikio kusikia wanacholalamika wananchi.

"Wananchi wana hali ngumu, sisi tuliozunguka na kuzungumza nao tunajua, biashara zinafungwa, wananchi masikini hali zao zimezidi kuwa ngumu, watumishi hawajapandishiwa mishahara hivyo hali kuzidi kuwa duni kwa wanaotegemea kuchuuza bidhaa kwa sababu hakuna anayemudu kununua," amesema Mbowe.

Amesema amani ya kudumu na demokrasia haiwezi kuwepo kama hakuna nafasi ya vyama vya siasa kufanya kazi zake bila kuonekana kama wahalifu.

Mbowe amesema wananchi wana kiu na shauku ya kuhudumia mikutano ya kisiasa.

Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post