MBUNGE WA CHADEMA AKAMATWA NA POLISI,WAMO MADIWANI WAWILI,MBUNGE MWINGINE ANASAKWA

Polisi mkoani Morogoro inawashikilia watu 41 akiwemo mbunge wa Mlimba (Chadema), Susan Kiwanga.


Pia inawashikilia madiwani wawili, huku mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali akitafutwa na jeshi hilo wakidaiwa kufanya fujo na kuchoma moto ofisi ya mtendaji baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Urlich Matei katika taarifa leo Jumatatu Novemba 27,2017 amesema tukio hilo lilitokea jana Jumapili Novemba 26,2017 saa tano usiku ambako walikwenda kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa udiwani.


Kamanda Matei amesema wabunge hao na madiwani wawili wa Chadema kutoka Ifakara walionekana kuhamasisha baadhi ya wafuasi wao kufanya vurugu.


Amesema watuhumiwa wanadaiwa kuchoma majengo ya umma ambayo ni ofisi shule ya msingi Sofi, nyumba ya walimu wa shule hiyo na ofisi ya mtendaji kata.


Kamanda Matei amesema fujo na uharibu huo ulitokea baada ya msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo kuwa mgombea wa CCM ndiye alishinda kwa kupata kura 2,099.


Mgombea wa chadema alipata kura 1,684 jambo lililopingwa na wafuasi wa chama hicho na kuanza vurugu.


Amesema baada ya kuchoma majengo hayo kwa kutumia petroli, walidhamiria pia kwenda katika zahanati lakini askari waliwakamata.


Kamanda Matei amesema polisi inaendelea kuwatafuta watu wengine waliohusika na vurugu hizo, akiwemo mbunge Lijualikali.


Amesema watuhumiwa 41 wamepelekwa wilayani Ulanga kwa ajili ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.


Mbunge Lijualikali amesema wakati matokeo yakitangazwa alikuwa Ifakara.



“Baada ya kumalizika kampeni Jumamosi nilirejea Ifakara kwa hiyo sijui chochote kuhusu hizo vurugu na nashangazwa kuhusishwa na tuhuma hizo, lakini kama kweli natafutwa nitakwenda kujisalimisha polisi,” amesema Lijualikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post