Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MBUNGE WA TARIME JOHN HECHE AJISALIMISHA POLISI



Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche ameripoti Kituo Kikuu cha Polisi Mkoa wa Morogoro kuitikia wito wa jeshi hilo. 


Heche amefika kituoni hapo leo Jumatatu Novemba 20,2017 saa sita mchana. 


Wakati Heche akiwa kituoni hapo baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema wa Manispaa ya Morogoro walionekana wakizunguka maeneo ya kituo hicho.


Akizungumza kwa simu, Heche ameiambia Mwananchi kuwa atatoa taarifa ya kilichoendelea baada ya kutoka kituoni hapo. 


"Nipo na maofisa wa polisi naendelea kuhojiwa nikitoka nitazungumza zaidi," amesema Heche. 


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema Heche aliahidi kwenda kituoni hapo leo. 


Polisi walioelezwa kutoka mkoani Morogoro Ijumaa Novemba 17,2017 walifika eneo la Bunge na Heche alilieleza Mwananchi kuwa walimpatia wito kuwa anatakiwa kwenda kuhojiwa mkoani Morogoro.


Mbunge huyo alisema hajui kosa alilotenda, isipokuwa anatakiwa kuhojiwa kwa kauli alizotoa alipomsindikiza mbunge wa Kilombero (Chadema), Peter Lijualikali alipotoka gerezani.


Akizungumza na Mwananchi Jumamosi Novemba 18,2017 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema mbunge huyo alifanya mkutano wa hadhara wilayani Kilombero Aprili 8, 2017.


Kamanda Matei alisema wanamtafuta Heche kwa kosa la kutotii amri za viongozi na kufanya mkutano Kilombero na kutoa lugha ya matusi hivyo kutaka kusababisha vurugu.


Amesema tangu siku ya tukio jeshi hilo limekuwa likimtafuta mbunge huyo bila mafanikio ndipo lilipoamua kulishirikisha Bunge.


Polisi iliandika barua kwa Spika wa Bunge kumtaarifu kuwa mbunge huyo anatafutwa kwenda kujibu tuhuma zinazomkabili mkoani Morogoro.

Imeandikwa na Hamida Shariff, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com