Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (MOI) imeokoa zaidi ya shilingi Bilioni 5 ambazo zingetumika kusafirisha wagonjwa nje ya nchi kufuata matibabu baada ya MOI kuanzisha huduma za kibingwa ambazo awali zilikua hazipatikani hapa nchini.
Hayo yamebainishwa katika ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii , Jinsia Wazee na watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya alipotembelea MOI na kukagua hali ya utoaji wa huduma, mazingira , miundombinu na kuwajulia hali wagonjwa pamoja na kukutana na menejimenti.
Akizungumza na menejimenti ya MOI, Dkt. Ulisubisya amepongeza kazi nzuri na kubwa inayofanywa ambayo imepelekea watanzania kupata huduma bora za kibingwa ambazo wangepaswa kuzifuata nje ya nchi.
“Mnafanya kazi nzuri sana, jambo ambalo linatupa faraja kubwa sisi viongozi wenu, naomba muongeze ubunifu zaidi, hamtakiwi kuifikiria MOI kwenye ukanda huu wa Afrika pekee bali duniani, hii ni changamoto kwetu sote kuifikisha hapo ”alisisistiza Dkt. Ulisubisya
Aidha, Dkt Ulisubisya amesema MOI imepunguza rufaa za kwenda nje ya nchi kwa asilimia 95% na asilimia 5% iliyobaki MOI inaweza kuimaliza kabisa na kusiwepo mgonjwa wa kwenda nje ya nchi.
Pia, amewaelekeza viongozi wa MOI kushirikiana na Wizara ya Afya kutafuta namna ya kufuta rufaa kwa kutoa mapendekezo na ushauri utakaosaidia kutatuliwa kwa changamoto hiyo.
“Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt John Pombe Magufuli ni kuhakikisha huduma zote za Afya zinapatikana hapa nchini na vyema sote tukamuunga mkono” amebainisha Dkt. Ulisubisya.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Profesa Muhamed Kambi amepongeza uongozi wa MOI kwa kuwa na maono ya mbali ya kuifanya MOI kuwa Taasisi bora barani Afrika na Duniani.
“Nimefurahi kwamba MOI mna maono ya mbali, mnafikiria kuitoa Taasisi hii hapa ilipo na kuifikisha sehemu ya juu zaidi, dira yenu ni kuwa Taasisi bora Afrika kufikia 2022 fanyeni kazi kwa bidii kufikia lengo hilo.” amesema Prof Muhamad Kambi
Awali akiwasilisha taarifa ya Utendaji, Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dkt Respicious Boniface amesema toka kuanzishwa kwa Taasisi hiyo imefanikiwa kuanzisha huduma za kibingwa za Upasuaji wa Nyonga, Magoti, Ubongo, Mgongo, Vibiongo, Usingizi ambazo zimesaidia kupunguza rufaa za nje ya nchi.
“Baada ya kuanzisha huduma hizi za Kibingwa tumefanikiwa kuokoa shilingi Bilioni 5 ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi, tumepunguza rufaa kwa asilimia kubwa naomba nikuhakikishie hata hizi asilimia 5% zilizobaki tutashirikiana na Serikali na naamini zitakwisha kabisa.” amesema Dkt. Respicious Boniface.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Dkt Mpoki Ulisubisya akizungumza na menejimenti ya MOI (hawapo pichani) katika ukumbi wa Mikutano wa MOI.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya akimjulia hali mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji mkubwa wa mgongo, anayetoa ufafanuzi wa namna upasuaji huo ulivyofanyika ni Dkt. Nicephorus Rutabansibwa (Daktari bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mgongo). Kushoto ni Mganga mkuu wa Serikali Profesa Muhamed Kambi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Dkt Mpoki Ulisubisya akikagua mashine mojawapo katika benki ya damu ya MOI
Mtaalamu wa Maabara Bwana Mbuta Jackson akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Dkt Mpoki Ulisubisya kuhusu namna benki mpya ya damu inavyofanya kazi kwa kushirikiana na Mpango wa Taifa wa damu salama
Watumishi wa MOI wakifuatilia hotuba ya katibu Mkuu Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii , Jinsia , Wazee na Watoto ( Sekta ya Afya) Dkt. Mpoki Ulisubisya (hayupo pichani) katika ukumbi wa Mikutano MOI.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Dkt Mpoki Ulisubisya akitoa maelekezo alipokua anakagua maeneo ya utoaji huduma katika jingo jipya la MOI (MOI phase III).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ,Maendeleo ya Jamii ,Jinsia , Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya ( katikati ) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya MOI.
( Picha zote na MOI ).
Social Plugin