MSIMU mpya wa kilimo cha pamba 2017/18 katika Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Tabora, Mara, Kagera, Singida, Kigoma na Katavi, umezinduliwa rasmi kwa upandaji pamba utakaoendelea hadi mwishoni mwa mwezi ujao.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika kijiji cha Mwamashimba wilayani Igunga mkoani Tabora jana, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marco Mtunga alisema katika msimu wa kilimo wa 2017/18 jumla ya tani 25,000 za mbegu zimetengwa, zikijumuisha tani 11,548 za mbegu mpya ya UKM08 na tani 13,452 za mbegu ya UK91.
Alisema kiasi hicho cha mbegu kinawahakikishia wakulima uwepo wa mbegu za kutosha kwa maeneo yote yatakayozalisha pamba kwa msimu huu wa kilimo na kuongeza kuwa hadi Novemba 12, mwaka huu, jumla ya tani 11,056 ambayo ni sawa na asilimia 70 ya mbegu zote zilikuwa zimesambazwa katika maeneo mbalimbali, ikiwa ni kati ya tani 15,694 zilizopangwa kusambazwa katika mgao wa awali.
Aliongeza usambazaji wa mbegu ulianza Septemba 15, mwaka huu na ukitarajiwa kukamilika Novemba 30, mwaka huu, ambapo jumla ya ekari 1,300,000 zinatarajiwa kupandwa katika msimu wa kilimo kwa mwaka huu.
Mtunga alisema serikali kwa kushirikiana na wadau imefanikiwa kufufua mfumo wa kuzalisha mbegu bora za kupanda na kwamba azma yake ya kuwapatia wakulima mbegu bora mpya ya UKM08 ifikapo mwaka 2018/2019 itatekelezwa kama ilivyopangwa.
Alisema mfumo wa uzalishaji wa mbegu bora za pamba unaanzia Kituo cha Utafiti cha Ukiriguru ambapo mbegu mama huzalishwa na baada ya kupatikana zinapelekwa kupandwa katika shamba la Nkanziga lililopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza kwa lengo la kuzalisha mbegu za awali.
Chanzo-Habarileo
Social Plugin