Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NEC KUFANYA UCHAGUZI SARANGA LICHA YA MOTO KUUNGUZA OFISI YA KATA




Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Saranga iliyopo Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam utafanyika Novemba 26, 2017 kama ilivyopangwa, licha ya kuteketea kwa moto vifaa vingi vya uchaguzi baada ya jengo la ofisi ya kata hiyo kuungua usiku wa kuamkia leo.

Kaimu Mkurungenzi wa uchaguzi (NEC) Hamis Mkunga amesema hayo leo baada ya kutembelea eneo la tukio na kueleza kuwa tayari ofisi yake imekwishafanya taratibu nyingine ili kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vilivyoteketea kwa moto vinapatikana na kusisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa.


“Tumefika hapa baada ya kupata taarifa za kuungua kwa jengo la Ofisi ya Kata ya Saranga ambalo pia tulihifadhi vifaa vya uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika jumapili ( Novemba 26, 2017) na bahati mbaya vifaa vingi vya uchaguzi vimeteketea vikiwemo rakili, vituturi, fulana na fomu mbalimbali, hata hivyo tayari tumefanya utaratibu wa kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana na uchaguzi unafanyika kama ilivyopangwa awali ” alisema Mkunga.

Aidha alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni hujuma kwani mashuhuda walipofika eneo la tukio walikuta dumu la mafuta ya petroli lakini hawajabaini sababu ya kutokea kwa hujuma hiyo na kuwa vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi zaidi.

Kuhusu hali ya usalama wakati wa uchaguzi Mkunga alieleza kuwa tayari vyombo vya usalama wilaya ya Ubungo vimejulishwa na kuwahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa usalama utaimarishwa na kuwataka wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.

Mkunga alisema bado hawajaweza kubaini kiwango halisi cha hasara kilichopatikana na kutokana na ajali hiyo na kuwa ofisi yake inaendelea kufanya tathmini juu ya hasara hiyo. 

Naye Mkuu wa Idara ya Uchaguzi NEC, Irene Kadushi amesema kata ya Saranga ina vituo vya kupigia kura 139 ambapo vifaa vyote vya uchaguzi awamu ya kwanza na ya pili vilikuwa vimekwishafika na kuwa awamu ya mwisho ya usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi katika kata hiyo ilikuwa ni jana asubuhi lakini walilazimika kuzuia upelekaji wa vifaa hivyo kutokana na tatizo hilo.

Aidha alisema  shughuli zote za uchaguzi ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uchaguzi zimehamishiwa katika Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa usalama zaidi, na kusisitiza kuwa taratibu nyingine zinaendelea na uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa.

Na Subira Kaswaga-NEC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com