Aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amemjibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kuhusu tuhuma ambazo amezitoa juu yake wakati akizungumza bungeni jana Novemba 13, 2017.
Nyalandu andika katika mtandao wa kijamii wa Instagram kuwa anasikitishwa na namna Dkt. Kigwangalla anavyotumia muda mwingi kumchafua mara baada ya yeye kutangaza kujivua uanachama wa CCM na kauli anazotoa dhidi yake ni za uongo.
Nyalandu ameandika;
INASIKITISHA sana kuona WAZIRI Kigwangalla akitumia MUDA wake ndani ya BUNGE leo kunichafua, kunidhihaki, na kusema UONGO na UZUSHI dhidi yangu, ikiwa ni NJAMA za makusudi zilizopangwa kunichafua mara baada ya mimi kukihama Chama Cha Mapinduzi -CCM. Aidha, hatua hiyo imepangwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa hakuna kiongozi yeyote wa CCM atakayethubutu ama kudiriki tena kukihama Chama Cha Mapinduzi CCM katika Serikali hii ya awali ya tano. AIDHA, Waziri Kigwangalla anatumika VIBAYA, kwa kauli za UONGO na UZUSHI aliuanza DHIDI yangu mara tu alipoteuliwa, kwa kuanza kutoa kauli za kejeli dhidi ya UTUMISHI wangu uliotukuka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na wenye REKODI thabiti.
NIANZE na UZUSHI alioutoa Waziri Kigwangalla mapema leo BUNGENI, huku moyoni mwake akiwa anajua fika kuwa ametumwa kusema UONGO dhidi ya Waziri Nyalandu kwa lengo la kuandaa MAZINGIRA ya kumkamata na kubwa zaidi, kudhalilisha azma ya WATANZANIA ambao WAKO tayari kwa mabadiliko ya UONGOZI wa nchi kupitia UPINZANI. AIDHA, propaganda za Kigwangalla ameamua zimuhusu Waziri moja tu wa Maliasili, tangu TAIFA kupata Uhuru. Waziri huyu ni Nyalandu, jambo linalothibitisha NJAMA na Progaganda za kuzimisha MOTO na nguvu ya umma kupitia UPINZANI, hasa baada ya kitendo changu Cha kukihama CCM.
1) WAZIRI Kigwangalla amekejeli kuwa Waziri Nyalandu alitumia Fedha za Serikali kusafiri USA na mwanadada Aunt Ezekiel. -HABARI hii ilikuwa ya KUZUSHA na ilichunguzwa na vyombo vya dola 2014 na kuthibitika ilitungwa na ilikuwa ya UONGO. Katika Mkutano huo wa Washington, DC, Waziri Nyalandu alialikwa na Balozi wa Tanzania, Marekani, na alipewa RUHUSA ya maandishi na Serikali kuhutubia Mkutano huo kwa siku Moja. Wasanii wote
Walioalikwa, akiwepo Mwanadada Aunt Ezekiel, hawakuwa na mwaliko wa Wizara ama Serikali, bali waandaji wa Kongamano. Na Serikali haikulipa gharama zozote kwao.(Mthibiti Na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anaweza kuthibitisha)
2) Waziri Kigwangalla amedanganya BUNGE kuwa Waziri Nyalandu alitumia helikopta kugombea URAIS 2015.
-Habari hii ni ya uzushi na UONGO, na Waziri atakuwa aidha hana BUSARA ambayo angepaswa kujiridhisha na Taarifa kabla ya kuisoma Bungeni, ama waliomtuma wamemwambia ASOME TU hivyo hivyo. UKWELI ni kuwa, Waziri Nyalandu, alipokuwa CCM, aligombea katika kinyang’anyiro cha URAIS kuomba kuteuliwa ndani ya CCM, na alitumia aidha usafiri wa MAGARI au NDEGE za kawaida kwa kulipa nauli (fixed wings pale ilipobidi), hadi mchakato ulipoisha kama uilivyoisha.
-AIDHA, miaka yote nikiwa Mbunge wa Singida Kaskazini, nimekuwa nikifanya kampeni za kumalizia kwa njia ya helikopta. Inawezekana Waziri Kigwangalla haelewi hili, lakini naomba nimjulishe TU kuwa matumizi ya helicopta ilipobidi yalisaidia kufika baadhi ya maeneo Jimboni kwangu wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2000, 2005, 2010, na 2015.
-AIDHA, Mwaka 2015 nilitumia Helicopter kwa SIKU TATU za kumalizia Kampeni, na nilikodi helikopta hiyo kwa Sh milioni tano kwa siku (Jumla, milioni 15)
-Pia ingependeza kama hamaki za Kigwangalla zingemkumbusha kuwa Waziri Nyalandu akiwa Wizarani ALIPATIA Serikali Helikopta mpya Moja, alileta ndege kwa matumizi ya kupambana na Ujangili, Alishawishi Benki ya dunia, Ujerumani na USA kuleta mamilioni ya dola za kmarekani kusaidia mapambano hayo, na kwamba alifanikiwa Sana kutokmeza ujangili nchini. RAIS KIKWETE alikiri hili wakati wa kuzindua Tangazo la Tanzania (Tanzania, the soul of Africa). 3) Kigwangalla amezusha kuwa Waziri Nyalandu alitumia vibaya madaraka yake. Amezungumzia suala la Waziri Nyalandu kutotia sahihi TOZO mpya zilizopendekezwa na TANAPA. Jambo ambalo Waziri Kigwangalla angepaswa kulijua kabla ya kutoa kauli isiyo sahihi Bungeni ni kuwa SAKATA la TOZO za Tanapa lilijadiliwa BUNGENI mbele ya Spika Mama Anne Makinda, likiwa limeletwa na Kamati ya Lembeli, na kwa kupitia Wizara, Waziri Nyalandu alilitolea ufafanuzi na likamalizika na GN ilitolewa.
-SAKATA la kupandishwa ghafla kwa TOZO za mahotelini zinazojulikana kama (Fixed Rates) lilianza kabla sijawa Waziri. Aidha, kulikuwa na kesi Mahakama Kuu, ambako hadi kufikia mwaka 2012, uamuzi wa Mahakama uliyotolewa. Bado Nyalandu hakuwa Waziri. Aidha, nilipoteuliwa kama Waziri, Nikatazama SAKATA hilo ambalo lilishachukua muda mrefu sana hadi kufikia 2014, mimi nilipokuwa Waziri. Sheria inasema ”Concession Fees shall be 10% of half Board”, na kulikuwa Na GN ya Serikali kuhusu TOZO hizo, takribani kuanzia mwaka 2002. Hukumu ya Jaji wa Mahakama Kuu ilielekeza kuwa TOZO zozote mpya ni sharti zipate GN mpya, na sheria ya msingi ilitaka TOZO ziwe kwa asilimia (percentage), na sio TOZO za kukisia, (fixed rate) ambazo ndio msingi mkubwa wa kupendeleana na rushwa katika kupanga nani alipe kiwango gani Cha kodi. Baada ya kuitolea maelezo Bungeni (na hansardi Zipo), Bunge na Wizara tulikubaliana namna ya kulimaliza na ndivyo ilivyofanyika na GN ilitolewa. Uamuzi wangu kama Waziri ulizingatia matakwa ya sheria na Kanuni. Waziri Kigwangalla hajasema ukweli na amezusha kuhusu suala hili kwa sababu anazozijua mwenyewe.
4) Sakata la VITALU: Inasikitisha SANA na inatia AIBU kwamba Waziri atalihadaa BUNGE kwamba Waziri Nyalandu amehusika na kuuza VITALU au kugawa VITALU, na baya Zaidi kwa NJIA ya RUSHWA. -Sheria ya Wanyamapori inatamka wazi kuwa VITALU vitagawiwa kwa wawindaji kwa kila baada ya miaka MITANO. -Mara ya mwisho VITALU vimegawiwa Januari, 2017. Nyalandu hakuwa WAZIRI. (Waziri alikuwa Mh. Prof Maghembe)
-Kabla ya hapo, VITALU viligawiwa mwaka 2013. Nyalandu hakuwa Waziri. (Waziri alikuwa Mh Maige)
Hii ni AIBU sana na natumaini kwa Waziri Kigwangalla na wanaomtuma wangetamani sana miaka ibadilike ili isomeke Waziri Nyalandu.
5) Waziri Kigwangalla amedai kuwa Waziri Nyalandu alikuwa anafanyia Kazi katika Chumba maalumu katika hoteli ya Serena. Naomba Waziri Kigwangalla, athibitishe ni Chumba namba ngapi, na wahusika wa hoteli pia wathibitishe. Kama Waziri, nilifanya Kazi katika ofisi yangu iliyopo Wizaranya Maliasili na Utalii. Kigwangalla pia akumbuke mimi nilikuwa MTEULE wa Rais ambaye alikuwa na vyombo vya kumsaidia kusimamia Mawaziri.
6) MADAI kuwa Waziri Nyalandu ALIUZA Twiga mwaka 2011/12 ni ya AIBU, UZUSHI na UONGO kuzidi shetani mwenyewe. Mwaka 2011/12 Nyalandu alikuwa NAIBU WAZIRI wa VIWANDA na BIASHARA! Uongo huu ni wa aibu na ni kazi ya Shetani Lusifa mwenyewe, na MUNGU wa mbinguni awakemee wote wanaohusika.
7) Mbwembwe hizi na kusingiziwa kunakofanywa kwa makusudi baada ya mimi Nyalandu kukihama CCM ni aibu kwa TAIFA na ni matumizi mabaya sana ya MADARAKA. Aidha, ifahamike kuwa Vitisho na njama dhidi yangu na familia yangu kunakofanywa na wote wanaohusika hakutazimisha azma ya watanzania kutaka mabadiliko ya kweli nchini. Imeandikwa, WAONGO wote, sehemu yao ni katika ziwa liwakalo moto kwa kiberiki. Haki huinua Taifa, na uonevu na dhuluma ni dhambi itakayowatafuna wahusika siku zote za Maisha yao.
— —— ——
Lazaro S. Nyalandu
Social Plugin