Shirika la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI limetoa warsha kwa Waviu Washauri kutoka mkoa wa Mwanza ili kuwajengea uwezo kwa ajili ya kuboresha huduma katika vituo vya tiba na matunzo (CTC).
Warsha hiyo ya siku tatu iliyoanza siku ya Jumanne Novemba 28,2017 katika ukumbi wa JB Belmont Hotel jijini Mwanza imekutanisha WAVIU washauri kutoka halmashauri za wilaya za Ilemela,Kwimba,Magu,Buchosa,Misungwi,Sengerema na Nyamagana.
Waviu washauri ni watu wanaoishi na maambukizi ya virusi vya Ukimwi na wamejiweka wazi na huru kuwashauri watu wanaoishi na VVU katika nyanja mbalimbali ikiwemo ufuasi mzuri wa dawa, kutoa ushauri nasaha kwa wenzao,kujitolea kufuatilia na kufundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha sambamba na kuhamasisha Waviu kujiunga katika vikundi ili kusaidiana na kupunguza unyanyapaa.
Akizungumza wakati wa kufungua semina hiyo,Mgeni rasmi ambaye ni Mratibu wa watoa huduma za afya ngazi ya jamii mkoa wa Mwanza, Bi Esperance Makuza,(aliyemwakilisha Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Mwanza, alisema Waviu Washauri wanayo nafasi kubwa ya kuboresha huduma za afya kwenye vituo vya tiba na matunzo.
“Nyinyi ni viungo muhimu sana katika kuwaunganisha wateja na vituo vya kutoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU,hivyo mafunzo haya yatawafanya mpate ujuzi na uzoefu mzuri katika kuwahudumia wateja”,alieleza.
Naye Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona alisema shirika hilo linafanya kazi zaidi kwenye vituo vya huduma na limekuwa likijuhusisha zaidi na watoto.
Alisema shirika hilo sasa linatekeleza majukumu yake katika mikoa sita nchini ambayo ni Shinyanga,Simiyu,Mwanza,Geita,Tanga na Mara.
Mafunzo hayo yameandaliwa na shirika la AGPAHI kwa ufadhili Watu wa Marekani kupitia shirika la Centres for Disease Control and Preventation (CDC).
ANGALIA MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA WARSHA YA WAVIU WASHAURI MWANZA SIKU YA KWANZA
Mgeni rasmi, Mratibu wa watoa huduma za afya ngazi ya jamii mkoa wa Mwanza, Bi. Esperance Makuza,aliyemwakilisha Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Mwanza akifungua warsha ya siku tatu ya watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi mkoa wa Mwanza katika ukumbi wa JB Belmont Hotel jijini Mwanza Jumanne Novemba 28,2017.
Afisa Miradi Huduma Unganishi kwa jamii AGPAHI mkoa wa Mwanza, Cecilia Yona akielezea historia ya shirika la AGPAHI na shughuli zinazofanywa na shirika hilo nchini Tanzania.
Bi. Cecilia Yona alisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi lakini pia kuhakikisha kuwa huduma za afya zinatolewa kama inavyotakiwa.
Mwezeshaji katika warsha hiyo Gladness Olotu ambaye ni muuguzi msaafu aliyebobea katika fani ya Ushauri nasaha akitoa mada kuhusu namna ya kutoa ushauri nasaha.
Washiriki wa warsha hiyo wakifuatilia mada iliyokuwa inatolewa.
Mwezeshaji Gladness Olotu akiendelea kutoa mada ukumbini.
Washiriki wa warsha hiyo wakiigiza namna ya kutoa ushauri nasaha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.
Mshiriki wa warsha hiyo Herman Ngika kutoka wilaya ya Magu, akichangia hoja ukumbini.
Washiriki wakifuatilia kilichokuwa kinaendelea wakati wa semina hiyo.
Mratibu wa Baraza la taifa la watu wanaoishi na VVU (NACOPHA),kanda ya Mwanza,Bi. Veronica Joseph akitoa mada kuhusu hali ya maambukizi ya VVU nchini Tanzania na haki za watu wanaoishi na VVU.
Bi. Cecilia Yona akitoa mada ukumbini.
Mratibu wa watoa huduma ngazi ya jamii wilaya ya Magu, Bi Ngehu Bussu akichangia hoja wakati wa warsha hiyo.
Washiriki wakiwa ukumbini.
Mwezeshaji Bi. Sherida Madanka akitoa mada wakati wa warsha hiyo.
Washiriki wa warsha hiyo wakicheza mchezo wa igizo namna ya kuhudumia wateja katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog