Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Picha : MKUTANO MKUU WA MWAKA 2017 WA VITUO VYA TAARIFA NA MAARIFA WILAYA YA KISHAPU VINAVYOSIMAMIWA NA TGNP MTANDAO

Rahel Madundo akifurahia ushindi baada ya kutangazwa kuwa amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga-Picha na Kadama Malunde - Malunde1 blog.
***

Wanaharakati wa masuala ya kijinsia kutoka katika vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga vinavyosimamiwa na TGNP Mtandao wamefanya Mkutano Mkuu mwaka 2017 wa vituo vya taarifa na maarifa katika wilaya ya Kishapu ulioandaliwa na baraza la kituo cha taarifa na maarifa la wilaya hiyo.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza Novemba 4,2017 hadi leo Jumapili Novemba 5,2017 umefanyika katika ukumbi wa Sheli ya BM kata ya Maganzo wilayani Kishapu.

Mbali na mkutano huo kuhudhuriwa na viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa kutoka kata saba,pia umehudhuriwa na maafisa watendaji wa kata pamoja na baadhi ya madiwani kutoka wilayani Kishapu.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kupanga mikakati na kuendeleza vituo vya taarifa na maarifa na kuunda baraza la kituo la wilaya ambapo wajumbe wa mkutano huo walichagua viongozi wa mtandao wa wilaya ambao kazi yao ni kusimamia shughuli zote za vituo vya taarifa na maarifa kwa wilaya hiyo ya Kishapu.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa baraza la kituo cha taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu uliofanyika katika mkutano huo,John Myola alimtangaza bi Rahel Madundo (aliyekuwa mwenyekiti wa baraza hilo kipindi kilichopita) kuwa mwenyekiti wa baraza hilo kwa muda wa miaka miwili.

Pia alimtangaza Bi Kayaya Rashid kuwa makamu mwenyekiti,Peter Nestory kuwa katibu mkuu,Renatus Mahona katibu msaidizi,Hellen Samson mhasibu na Gayunga James,Pendo Michael,Scolastica Joseph na Agnes Lutamula kuwa wajumbe wa kamati ya utendaji.

Viongozi wengine ni Catherine Revocatus aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa vijana wilaya ya Kishapu,Suzana Yohana kuwa Katibu,Paul Masamaki kuwa mwakilishi wa kanda ya Mondo,Kulwa Jandikile kanda ya Negezi na Edward Charles kanda ya Kishapu.

Akizungumza katika mkutano huo,Afisa Programu – Ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka TGNP Mtandao,Deogratius Temba alisema vituo vya taarifa na maarifa vimesaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa matukio ya ukatili wa kijinsia.

“Tulianza harakati za kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani Kishapu mwaka 2012,katika maeneo ambapo kuna vituo vya taarifa na maarifa,jamii imejitambua ambapo wananchi wamejitambua na wamekuwa na ujasiri wa kupinga vitendo hivi lakini pia wanawake wamekuwa na ujasiri wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi”,alieleza Temba.

Temba alibainisha kuwa wanaharakati wa masuala ya kijinsia kwa kushirikiana na madiwani wamechangia kwa kiasi kikubwa kuihamasisha halmashauri ya wilaya ya Kishapu kuwa na bajeti yenye jicho la kijinsia.

“TGNP Mtandao inawapongeza sana viongozi wa vituo pamoja na madiwani kwa jitihada wanazofanya katika kuifanya halmashauri ya wilaya ya Kishapu kuwa mfano wa kuigwa katika kusimamia na kutetea masuala ya kijinsia”,aliongeza Temba.

Naye Mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu Rahel Madundo,alisema tangu kuanzishwa kwa vituo hivyo mwaka 2012 wilayani humo,wanaharakati wameisadia jamii kujitambua na kuanza kudai haki zote za binadamu pamoja na kuingia katika vikao vya kata (WDC).

“Akina mama wamejengewa uwezo wa kuongea kwenye mikutano ya hadhara na kuhudhuria mikutano mbalimbali kuomba nafasi za uongozi”,alisema Madundo.

Aidha alilishukuru shirika la TGNP Mtandao kwa kuwapatia elimu ya uraghabishi ambayo imewasaidia kujitambua huku akiliomba shirika hilo kuongeza vituo vingine katika wilaya hiyo kwani sasa vipo saba pekee.

Katika hatua nyingine aliiomba halmashauri ya wilaya ya Kishapu kuvipatia mikopo vituo vya taarifa na maarifa kwa ajili ya kujiendesha na kuanzisha miradi.

Nao wajumbe wa mkutano huo walikubaliana kuwa kila shule ya msingi wilayani humo iwe na chumba maalumu kwa ajili ya watoto wa kike kujisitiri wanapokuwa katika hedhi ambapo waliahidi kushiriki katika ujenzi wa vyumba hivyo.

Kwa upande wake,Mkurugenzi wa shirika linajihusisha na masuala ya haki za watoto na wanawake la Agape Aids Control Programme,John Myola aliyealikwa kushiriki mkutano huo,aliwataka viongozi wa vituo vya taarifa na maarifa na madiwani kuendeleza ushirikiano walionao katika kuwatetea watoto na wanawake na kuepuka kutumiwa na wanasiasa wenye nia mbaya.

“Bado matukio ya ukatili wa kijinsia yapo,watoto wanabakwa,wanapewa mimba,tafadhali fanyeni kazi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi katika kutetea wanyonge,kuweni na ushirikiano,tunzeni siri ili kutowapa mwanya wahalifu,lakini pia jitahidini kutoa taarifa mahali panapohusika kwa wakati”,alieleza Myola.

Naye Diwani wa kata ya Mwaweja,Makanasa Kishiwa alilishukuru shirika la TGNP mtandao kwa kuichagua halmashauri ya Kishapu kuwa miongoni mwa halmashauri 28 ambako vituo vya taarifa na maarifa vimeanzishwa na kuahidi kuwa madiwani wataendelea kuungana na shirika hilo katika jitihada za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia. 

Harakati za TGNP Mtandao wilayani Kishapu zilianza mwaka 2012 katika kata ya Songwa na baadae kuzaa vituo vya Kishapu,Mondo,Ukenyenge,Mwaweja,Mwadui Lohumbo na kata ya Maganzo na mpaka sasa kuna jumla ya vituo 7 katika wilaya hiyo.

Lengo kuu la kituo cha taarifa na maarifa ni kutoa elimu kwa jamii nzima,zikiwemo elimu ya kudai rasilimali za umma,ukatili wa kijinsia,mimba za utotoni na haki za binadamu.

ANGALIA PICHA ZA MATUKIO HAPA CHINI



Afisa Programu – Ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka TGNP Mtandao,Deogratius Temba akizungumza katika Mkutano mkuu mwaka 2017 wa vituo vya taarifa na maarifa katika wilaya ya Kishapu leo Jumapili Novemba 5,2017 katika ukumbi wa sheli ya BM uliopo katika kata ya Maganzo wilayani Kishapu.Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog
Afisa Programu – Ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka TGNP Mtandao,Deogratius Temba akiwasisitiza wanaharakati wa masauala ya kijinsia kuongeza nguvu kukabilina na vitendo vinavyokiuka haki za binadamu
Wajumbe wa mkutano wakiwa ukumbini
Afisa Programu – Ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka TGNP Mtandao,Deogratius Temba
Mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu Rahel Madundo akizungumza katika mkutano mkuu  mwaka 2017 wa vituo vya taarifa na maarifa katika wilaya ya Kishapu.

Wajumbe wa mkutano wakimsikiliza Mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu Rahel Madundo
Aliyekuwa katibu wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu  Samwel Kalima akizungu
Diwani wa kata ya Mwaweja,Makanasa Kishiwa akizungumza katika mkutano ambapo alilishukuru shirika la TGNP mtandao kwa jitihada mbalimbali linalozifanya katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani Kishapu
Diwani wa viti maalumu kata ya Bunambiyu Helena Paul akizungumza ukumbini ambapo alisema vituo vya taarifa na maarifa vimewasaidia wanawake kujitambua na sasa kuna viongozi wanawake katika ngazi mbalimbali wilayani humo wakiwemo madiwani waliochaguliwa katika uchaguzi mkuu uliopita waliowagaragaza wanaume katika uchaguzi huo mkuu wa mwaka 2015
Afisa Mtendaji wa kata ya Ukenyenge,Chief Ng'ombe akizungumza kwa niaba ya maafisa watendaji wilayani humo ambapo aliwataka wanaharakati wa haki za binadamu kuendelea kushirikiana na serikali katika kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia
Mwenyekiti wa Mkutano huo,Abdul Mohammed Ngolomole ambaye ni diwani wa kata ya Songwa akimkaribisha Mkurugenzi wa uchaguzi wa baraza la kituo cha taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu uliofanyika katika mkutano huo,John Myola ili kutoa utaratibu wa namna ya kuchagua viongozi wapya wa baraza la kituo la wilaya ya Kishapu.
Kulia ni Mwenyekiti wa Mkutano huo,Abdul Mohammed Ngolomole ambaye ni diwani wa kata ya Songwa akimkabidhi vifaa vya uchaguzi Mkurugenzi wa uchaguzi wa baraza la kituo cha taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu,John Myola
Mkurugenzi wa uchaguzi wa baraza la kituo cha taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu ,John Myola akizungumza wakati wa kutangaza majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali katika baraza hilo
Mkurugenzi wa uchaguzi wa baraza la kituo cha taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu ,John Myola akielezea utaratibu wa kupiga kura
Wasimamizi wa uchaguzi wakigawa karatasi za kupigia kura baada ya wagombea wa nafasi mbalimbali ( hawapo pichani) kuomba kupigiwa kura
Wajumbe wa mkutano wakiweka kura zao kwenye ndoo
Rahel Madundo akifurahia ushindi baada ya kutangazwa kuwa amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu kwa kipindi kingine cha miaka miwili
Rahel Madundo akiwashukuru wajumbe wa mkutano huo kumchagua tena kuwa Mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu 
Bi Kayaya Rashid akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua kuwa makamu Mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu.Kushoto ni Hellen Samson aliyechaguliwa kuwa mhasibu,kulia ni Rahel Madundo aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa vituo vya taarifa na maarifa wilayani humo.
Peter Nestory akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua kuwa katibu mkuu wa vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu.
Picha ya pamoja: Viongozi waliochaguliwa kuongoza baraza la vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu
  Viongozi wa baraza la vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu
Picha ya pamoja: Viongozi waliochaguliwa kuongoza baraza la vituo vya taarifa na maarifa wilaya ya Kishapu,madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Afisa Programu – Ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka TGNP Mtandao,Deogratius Temba na Mkurugenzi wa shirika la AGAPE John Myola
Picha ya pamoja : Madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Kishapu,Afisa Programu – Ujenzi wa nguvu ya pamoja kutoka TGNP Mtandao,Deogratius Temba na Mkurugenzi wa shirika la AGAPE John Myola.
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com