Kufuatia mvua za masika zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali mkoani Rukwa radi iyopiga juzi imeua papo hapo ng’ombe kumi waliokuwa malishoni huku mchungaji wa wanyama hao Ahmad Katunzi (15) akinusurika kufa.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Rukwa , George Kyando amethibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotokea jana saa kumi na moja jioni katika kijiji cha China kilichopo katika Kata ya Kate wilayani Nkasi.
Akisimulia mkasa huo mwenyekiti wa kijiji hicho,Joseph Ndasi ambaye pia ndiye mwenye mifugo hiyo alisema Ahmad alikuwa akichunga ng’ombe wapatao 22 ambapo ghafla radi ilipiga na kuua ng’ombe kumi papo hapo.
“Katika tukio hilo mchungaji Ahmad alijikuta amerushwa takribani mita kumi kutoka alipokuwa amesimama na amepata majeraha madogo madogo … ngombe wengine kumi na mbili wamenusurika ila kwa hofu wote walikimbia na kurejea nyumbani “ alieleza .
Taarifa kutoka kijijini zinakumbusha usemi wa wahenga usemao kufa kufaana kwani wakazi wake walivamia mizoga ya wanyama hao na kuanza kugawana nyama yake.
Na Walter Mguluchuma -Malunde1 blog Nkasi
Social Plugin