Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS MAGUFULI AMTUMIA RAMBIRAMBI SPIKA NDUGAI KIFO CHA MBUNGE GAMA







Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemtumia rambirambi Spika wa Bunge, Job Ndugai kutokana na kifo cha mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama.

Gama amefariki dunia jana Alhamisi Novemba 23,2017 saa 4:25 usiku katika Hospitali ya Misheni ya Peramiho, iliyopo wilayani Songea mkoani Ruvuma alikopelekwa kwa matibabu baada ya kuugua ghafla.

Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu leo Ijumaa Novemba 24,2017 Rais Magufuli amesema amepokea kwa mshtuko na majonzi taarifa za kifo cha Gama.

“Nakupa pole Spika Ndugai, wabunge na wafanyakazi wa ofisi yako; na kupitia kwako naomba ufikishe salamu zangu za pole kwa familia ya marehemu, wananchi wa jimbo la Songea Mjini na mkoa wa Ruvuma, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu,” amesema Rais Magufuli.

Amempa pole pia mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho na wana CCM kwa kumpoteza kada aliyekiwakilisha vyema chama hicho kwa nafasi yake ya ubunge.

Rais Magufuli amesema Gama aliyewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo ukuu wa wilaya, mkoa na ubunge alikuwa kiongozi hodari, aliyefanya kazi kwa kujiamini na aliyependa kupigania masilahi ya wananchi bila kuchoka.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com