Muonekano wa Noah baada ya ajali
***
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi kufuatia vifo vya watu 12 vilivyosababishwa na ajali ya magari mawili kugongana uso kwa uso.
Ajali hiyo imetokea tarehe 23 Novemba, 2017 majira ya saa 2:30 usiku katika eneo la Ighuka Wilaya ya Ikungi, Mkoani Singida ambapo basi dogo aina ya Toyota Hiace lililokuwa limebeba watu waliotoka kwenye sherehe ya harusi limegongana na gari dogo aina ya Noah lililokuwa linatoka msibani.
Katika salamu hizo Mhe. Rais Magufuli amemtaka Dkt. Rehema Nchimbi kufikisha salamu zake za pole kwa familia zilizopoteza jamaa zao, ndugu na marafiki.
“Ajali hii imeleta majonzi makubwa sio tu kwa familia zilizopoteza jamaa zao bali kwetu sote, tumepoteza ndugu zetu wengi ambao wameacha familia zao, wapendwa wao na jamaa waliowategemea, kwa hakika hili ni pigo kubwa”
“Naungana na familia za Marehemu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na pia nawaombea Marehemu wapumzike mahali pema, wote walioguswa na vifo hivi wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amevitaka vyombo vinavyosimamia matumizi ya barabara na usalama barabarani, kuongeza juhudi katika udhibiti wa ajali na kuwachukulia hatua kali wote wanaovunja sheria na kusababisha ajali.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
24 Novemba, 2017