Ndege hiyo ni miongoni mwa ambazo Serikali iliahidi kuzinunua ikiwa ni mikakati ya kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
Mpaka sasa, ndege mbili aina Bombardier zenye uwezo wa kubeba abiria 75 zimeshanunuliwa na zinaendelea kutoa huduma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu miaka miwili ya utawala wa Rais Magufuli ulioingia madarakani Novemba 5, 2015, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema itakapokamilika itakuja nchini na kwamba kufikia Juni mwakani zote zitakuwa zimewasili isipokuwa moja itakayokuja Julai.
Alisema hayo baada ya kuulizwa na mwandishi kuhusu ujio wa ndege hiyo iliyokuwa iwasili miezi minne iliyopita.
“Tunanunua ndege nne… kwa sababu moja ya malalamiko makubwa sana huko nyuma ilikuwa ni lawama kuhusu shirika letu la ndege kwamba huwezi kuwa na nchi yenye vivutio vyote hivi vya utalii lakini huna shirika imara la ndege.
“Kwa hiyo tumeanza hizo juhudi na mimi nasema kufikia mwakani ndege zote za awamu hii tulizoziagiza zitakuja nchini na ndege hiyo uliyoitaja itakuja nchini, iko katika majaribio si kama baiskeli unaweza kufunga tairi na kuanza kutumia,” alisema Dk Abbasi.
Alisema, “Kuna vipimo, kuna viwango vya kimataifa kufikiwa, ila ninachosema kwa sasa inafanyiwa ukaguzi itakapokamilika itakuja nchini ila kufikia Juni mwakani zile ndege zote. Ile kubwa Boeing 787 yenye uwezo wa kubeba abiria 262 itakuwa imewasili ifikapo Julai mwakani.”
Kuchelewa kuwasili kwa ndege hiyo kuliibua mjadala mkubwa baada ya Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu Agosti 18 kuitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kudai kwamba ndege hiyo imekamatwa na inaweza kupigwa mnada kwa deni inayodaiwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd ya Montreal, Canada.
Alisema kampuni hiyo iliishtaki Serikali katika Mahakama ya kimataifa, ikipinga kuvunjiwa mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo, jijini Dar es Salaam na ilitaka kulipwa fidia ya Dola 38 milioni za Marekani, sawa na zaidi ya Sh87 bilioni.
Hoja hiyo ya Lissu iliibua mjadala mkali sehemu mbalimbali na kumfanya kuitwa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kutoa maelezo ya alipozipata taarifa hizo.
Serikali Agosti 19, ilifanya mkutano na waandishi wa habari kukanusha taarifa hizo lakini ilikiri kuwapo kwa mgogoro.
Aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa aliwaambia waandishi wa habari kwamba kuna mgogoro kuhusu ndege hiyo ambao kimsingi umetengenezwa na Watanzania ambao kwa bahati mbaya wameweka masilahi ya kisiasa na ya binafsi mbele zaidi ya masilahi ya Taifa.
Zamaradi alisema Serikali ilikuwa imeanza majadiliano ya kidiplomasia kulimaliza sula hilo na kuwataka Watanzania kuwa watulivu wakati suala hilo linashughulikiwa.