Spika wa Bunge, Job Ndugai ametahadharisha kuhusu muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli wa Taifa wa mwaka 2017 kuwa ukipitishwa kama ulivyo, unakwenda kutengeneza udikteta.
Spika alitoa kauli hiyo muda mfupi kabla ya kusitisha shughuli za Bunge jana mchana baada ya wabunge kuchangia muswada huo wakiukosoa vikali.
Muswada huo uliowasilishwa na waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Mbarawa aliyesema unalenga kuanzishwa kwa Shirika la Wakala wa Meli litakalojulikana kwa kifupi Nasac.
Shirika hilo, pamoja na mambo mengine litakuwa na jukumu la kutoa huduma ya uwakala wa meli kwa maeneo mahsusi pamoja na kudhibiti huduma za usafiri na usalama wa vyombo vya majini.
Profesa Mbarawa alisema muswada huo unaweka mfumo madhubuti wa uendeshaji wa biashara ya uwakala wa meli na udhibiti ili kuimarisha sekta ndogo ya usafiri wa majini.
Hata hivyo, wabunge wamekosoa baadhi ya vifungu kwa vile vinaifanya Nasac kufanya biashara na hapohapo kuwa mdhibiti wa biashara hiyo kwa kampuni binafsi.
Upungufu wa muswada huo ndio uliomsukuma Spika Ndugai kutahadharisha juu ya mamlaka makubwa aliyopewa mkurugenzi mtendaji wa Nasac ikiwamo kufuta leseni za kampuni binafsi.
“Michango ya waheshimiwa wabunge ni muhimu sana mkaitazame, vizuri vinginevyo huyu mkurugenzi wa Nasac tunayemtengeneza hapa tutakuwa tunamtengeneza dikteta bila kujitambua,” alisema Ndugai.
“Kama kweli peke yake ana madaraka makubwa ingawa anaweza kuwa na vyombo lakini kama anapewa mamlaka makubwa kiasi hicho, kidogo itabidi kuliangalia vizuri.
“Uzuri wabunge wanaunga mkono ila wanataka marekebisho ya hapa na pale. Pale mtu anapewa mamlaka makubwa basi akumbushwe tu kuwa Mungu yupo na asifikiri kwamba yeye ni Mungu.”
Spika alisema kuna mambo matatu katika muswada huo ambayo anaona hayajakaa sawa likiwamo jina hilo la Nasac ambalo alisema linarudisha kumbukumbu ya Wakala wa Meli wa Taifa (Nasaco).
Nasaco iliwekwa katika orodha ya kubinafsishwa mwaka 1997 na kufungwa kabisa mwaka 2002 na nafasi yake kuchukuliwa na kampuni zaidi ya 30 ambazo zinafanya majukumu iliyokuwa nayo. “Jina kwa kweli tabu. Hata kama linarudi Nasac ndio Nasaco hiyohiyo. Nasaco ilikuwa tatizo. Inafanya hiki kitu kipya ni kama mtoto mzuri anaitwa Juma lakini anaitwa Juma Idd Amin,”alisema.
“Ile Idd Amin inaharibu huyu Juma pamoja na nia yake njema. Halafu hili la kwamba TRA (Mamlaka ya Mapato) ndio tatizo kubwa, nayo anashughulikiwaje na hili la mdhibiti mchezaji,” alisema Spika.
Katika mchango wake, mbunge wa viti maalumu (CCM), Esther Mmasi alisema si sahihi Serikali ikawa mdhibiti wa biashara za wakala wa shughuli za majini na hapo hapo ikawa mchezaji.
“Najiuliza kwamba Serikali itakuwa mdhibiti, itakuwa key player (mchezaji muhimu) lakini wakati huohuo itakuwa mdhibiti wa shughuli za wakala wa shughuli za baharini. Sielewi hapa,” alisema Esther.
“Mimi sipingani na Serikali na naunga hoja asilimia 100, lakini nitashukuru kupata mwelekeo ni nani atakuwa anafanya oversight function (majukumu ya usimamizi) kwenye muktadha mzima.”
Alisema mkurugenzi mkuu wa Nasac amepewa nguvu kubwa ya kutoa leseni na kufuta leseni za kampuni itakayokuwa inashindana nayo, jambo ambalo ni mgongano wa masilahi.
“Ni vyema tukaenzi kauli za Rais ambapo mara nyingi anapokutana na wawekezaji anajaribu kufanya fair environment (mazingira sawa) kwa ushiriki wa private sector (sekta binafsi),” alisema mbunge huyo.
“Maana yangu na kiu yangu ni kuona tunatengeneza mazingira rafiki ya ushiriki wa sekta binafsi. Yaani kusimamisha leseni ni yeye, yeye huyo huyo atapanga muda gani wa kuisimamisha.
“Yuko mtu aliwahi kutumia vibaya madaraka yake mwaka 2015 kuagiza mafuta, kwa madaraka kama hayahaya akaingiza Serikali kwenye hasara kubwa iliyoelekea kuwa ni uhujumu uchumi.”
Kwa upande wake, mbunge wa viti maalumu (CCM), Dk Immaculate Sware alitaka kujua kwa nini Nasaco ilifutwa na Serikali inakuja na sheria ya kuanzisha Nasac akisema uanzishwaji huo unaleta mgongano wa kisheria.
“Sheria inaleta utata katika kuzuia sekta binafsi kushiriki katika biashara hii. Inaweza kutoa leseni kwa mawalaka lakini inawabana kuwa hawawezi kusafirisha nyara za Serikali au madini,” alisema.
“Inaleta mkanganyiko kwamba huyu Nasac ndio atakuwa anasafirisha mwenyewe, anajisimamia mwenyewe na anajidhibiti mwenyewe. Kunakuwa na mgongano wa kimasilahi,” alisisitiza.
Mbunge wa viti maalumu (CUF), Rukia Kassim Ahmed alisema ingependeza Nasac ianzishwe baada ya kuwadhibiti baadhi ya maofisa wa TRA bandarini wasio waaminifu.
“Kwenye bandari zetu kuna upotevu mkubwa wa fedha na wizi unaotokana na TRA. Wizi na upotevu mkubwa ni kwa wenzetu wa TRA ambao ndio wanasababisha wizi huu,” alisema Rukia.
“Mtuambie Nasac, Serikali itaziba vipi mwanya huu wa upotevu wa fedha unaofanywa na watumishi wasio waaminifu wa TRA. Hiyo itasababisha Nasac kufanya kazi vizuri.” Mbunge huyo alisema wakati wanapokea maoni ya wadau, aliyekuwa mkurugenzi wa Sumatra aliwaambia kwamba aliwahi kusafirisha makontena sita akiambiwa ni majani ya chai, lakini kumbe ni bangi.
Hiyo ilifanyika kwa sababu sheria ilikuwa inawabana Sumatra wala Mamlaka ya Bandari (TPA), kiasi kwamba walikuwa hawawezi kujua kilichomo ndani ya makontena isipokuwa maofisa wa TRA.
“TRA ndio wali-take advantage (mwanya huo) kusafirisha mzigo huo. Mtuambie Nasac mtaziba vipi wizi huu na mchezo huu. Tufafanulieni watafanyaje wakati TRA bado ipo pale?” alihoji.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alisema CCM katika ilani zake kuanzia 1995 hadi 2015 ilisema itaendelea na ubinafsishaji na kuiachia biashara ishikwe na sekta binafsi. “Leo Serikali iliyojiondoa kufanya biashara inarudi kufanya biashara. Nasac kusajili na kutoa leseni na hapohapo yenyewe inafanya biashara, inaondoa dhana nzima ya ushindani na utawala bora,” alisema.
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Emanuel Mwakasaka alihoji kwa nini Serikali inapata ukakasi wa kuiita Nasaco kama ilivyokuwa nyuma wakati jina ni kama lilelile.
Pia alikosoa hatua ya Serikali kujiingiza katika kufanya biashara na hapohapo ikawa ndio msimamizi, na kusema hiyo ni sawa na Serikali kupiga mpira halafu ikacheza yenyewe.
Mbali na suala hilo, lakini mbunge huyo alisema hata Bunge litunge sheria nyingi kiasi gani kusimamia suala la biashara ya majini, haitakuwa na manufaa kama maofisa wa TRA hawatadhibitiwa.
Mbunge huyo alipendekeza kufungwa kwa kamera za CCTV katika maeneo yote muhimu bandarini, ili kudhibiti wizi na udanganyifu unaofanyika kwa kuwa utaonekana katika kamera hizo.
Imeandikwa na Daniel Mjema, Mwananchi
Social Plugin