BEKI kisiki wa kati na nahodha wa timu ya Lipuli FC, raia wa Ghana, Asante Kwasi, amesema yupo tayari kumwaga wino katika kikosi chochote, ikiwamo Yanga iwapo watakubali kukaa mezani na kufanya naye mazungumzo.
Kwasi aliwahenyesha Simba katika mchezo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, huku yeye akiwa ndiye aliyeisawazishia timu yake kwa mkwaju wa faulo mara baada ya beki wa Simba, Yusuph Mlipili, kumfanyia madhambi winga, Seif Karihe.
Beki huyo amekuwa katika kiwango bora tangu alipotua katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara akitokea Swaziland, alipokuwa akicheza soka katika kikosi cha Mbabane Swallows.
Mlinzi huyo wa kati ana mabao mengi kuliko mabeki wote msimu huu akiwa tayari amepachika mabao matano katika michezo 10 aliyoshuka dimbani.
Nyota huyo ameondoka nchini mara baada yakumaliza mchezo wake na Simba ambapo walitoa sare ya bao 1-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao ulichezwa juzi katika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza nasi, jijini Dar es Salaam, Asante alisema hivi sasa amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na Lipuli, lakini iwapo kama kuna timu yoyote itakayokuwa ikimhitaji inapaswa kuongea na waajiri wake.
“Mimi nipo tayari kutua katika timu yoyote ambayo itakuwa ikinihitaji itakayokuwa tayari kukubaliana na masharti yangu kwani mpira ni kazi yangu iliyonileta hapa nchini.
“Ni jambo zuri na linavutia kutakiwa na timu kubwa na yenye historia kubwa kama Yanga wenye mashabiki wengi nchini Tanzania,” alisema.
Alisema amekuwa akisikia tetesi mtaani za kutakiwa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, lakini hadi sasa hawajamfuata kufanya mazungumzo naye.