Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

USIYOYAJUA KUHUSU TAJIRI MTATA ALIYELETA GUMZO NYUMBA ZA LUGUMI...ADAIWA KUWA NI MSUKUMA WA SIMIYU

Wakati maswali mengi yakijitokeza kuhusiana na Dk. Louis Shika, ambaye aliibuka mshindi katika mnada wa nyumba za kifahari za Said Lugumi zilizoko Mbweni JKT na Upanga jijini Dar es Salaam kwa thamani ya jumla ya Sh. bilioni 3.3, imebainika kuwa anaishi katika chumba kimoja cha kupanga.


Imebainika kuwa Dk. Shika anakaa kwenye nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Amani kwa kipindi cha takribani mwaka mmoja sasa na kodi anayolipa kwa mwezi ni takribani Sh. 50,000.


Aidha, baadhi ya majirani zake wamemuelezea kuwa ni mtu asiye na makeke, huku baadhi wakidai kuwa aliwahi kuwaahidi wauza mihogo ya kukaanga walio jirani na mahala anapoishi kuwa atawaunganishia kupata mikopo nafuu ili wakuze biashara zao, lakini bila ya kuwatajia taasisi atakayowaunganisha nao. Inadaiwa kuwa vilevile, kwa baadhi ya watu hufahamika kwa jina la ‘profesa’.


Dk. Shika alijipatia umaarufu katikati ya wiki baada ya kuibuka mshindi katika mnada wa nyumba za kifahari za Lugumi, kwa kununua nyumba moja ya Mbweni kwa Sh. bilioni 1.2, nyumba ya pili iliyoko pia Mbweni Sh. milioni 900 na nyumba ya tatu iliyoko Upanga alishinda na kutaka kununua kwa Sh. bilioni 1.2.


Hata hivyo, alishindwa kutumiza masharti ya kulipa asilimia 25 ya fedha kwa kila nyumba baada ya kushinda, hivyo kujikuta akitiwa mikononi mwa vyombo vya dola kwa kuharibu mnada.



Katikati ya wiki hii, jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, lilimtia nguvuni Dk. Shika kutokana na tuhuma za kuharibu mnada huku likidai kuwa linafanya uchunguzi zaidi ili kubaini kwa nini alifanya hivyo.


Mbali na kuchunguza juu ya hatua ya kuharibu mnada, kamanda wa kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema walikwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi sambamba na kuchunguza udaktari wake. Shika aliwahi kukaririwa kuwa ni msomi wa shahada ya uzamivu (Ph.D).


Hata hivyo, Mambosasa alisema udaktari wake huo unatia shaka kwa kuwa ameshindwa kuonyesha vielelezo kuthibitisha kama anastahili hadhi hiyo.

Maoni ya mdau wa jamiiforums kuhusu Dr. Shika

Nimeguswa sana na tukio la kushikiliwa na vyombo vya dola mtu anayetajwa kama Dr Louis Shika (pichani) ukiacha tukio lilivyo, mtu huyo ninamfananisha sana na "SHIKA LUNYALULA KIDOLA" mzaliwa wa kitongoji cha CHAMUGASA kijiji cha KALEMELA wilaya ya BUSEGA, Simiyu.
Nimeona hata passport ya Dr.Louis Shika kwenye jina la ubin (surname) imeandikwa Kidola. Kwahiyo huenda ni yeye.
Shika ninayemfahamu, ni ndugu yake JEREMIAH SHIKA KIDOLA. Hawa wawili waliakuwa miongoni mwa wanafunzi wenye akili sana na waliofaulu vizuri masomo yao ya sekondari kwa alama za juu na kupata ufadhili wa kwenda kusoma udaktari nchini Urusi.
Walikuwa wanafunzi wa vyuo vikuu huko USSR (Urusi ya zamani) mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990, ambapo walirejea nchini na kuanza kutibu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili.
Nakumbuka wote wawili Dr.Louis na Dr.Jeremiah Shika (ambaye ni marehemu kwa sasa), walisoma udaktari bingwa huko Urusi. Dr.Jeremiah ndiye aliyetangulia kuwa daktari bingwa na aliporudi alifanya kazi kidogo Muhimbili na baadae aliajiriwa kuwa miongoni mwa madaktari bingwa (Specialist) wa mwanzomwanzo pale Bugando Hosptital Mwanza.
Dr.Louis yeye alihudumu kwa muda kama daktari wa kawaida (MD) kabla baadae hajaenda kujiendeleza zaidi nchini Urusi na kusomea udaktari bingwa. Sina hakika sana alispecialize kwenye nini lakini kama sikosei ni magonjwa ya akili (psychiatrist).
Binafsi nina zaidi ya miaka 30 bila kuonana na Dr.Shika, ingawa ilijulika mapema kuwa alioa mke wa Kirusi alipoenda kusoma masomo yake ya juu, na baadaye kuzama kwenye ulevi wa pombe za kupindukia huko Urusi.
Mwaka juzi nilikutana na mdogo wao Daudi Shika aishiye kijiji cha Mwamanga - Magu, akanijulisha kuwa, DR.SHIKA alisharudi Tanzania lakini alidai akili zake hazina utimamu tena.
Daudi akaniambia Dr.Shika alirudi nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000 lakini hawajui kama alihitimu masomo yake ya udaktari bingwa au alikatisha. Japo zipo taarifa kuwa hakuhitimu kutokana na ulevi wa kupindukia na akili yake kuonekana haiko sawa, na alirudishwa kwa amri ya serikali.
Kwahiyo ana zaidi ya miaka 15 tangu arudi nchini lakini kila siku anadai kusubiri mizigo yake kutoka Urusi ifike bandarini. Alinieleza kuwa kaka yao (Dr.Louis) alikuwa hajui kwa nini mizigo yake imechelewa kufika hali ambayo ilidaiwa kumsababishia msononeko mkubwa sana.
Daudi aliniambia kuwa ilikuwa zaidi ya miaka 12 tangu Baba yao mzee Lunyalula Kidola afariki dunia (mwaka 2005), lakini kaka yao Dr.Louis hakuwahi kufika msibani licha ya kuwepo Dar es Salaamu. Hata mawasiliano na ndugu zake kijijini ni kwa nadra sana na mara nyingi ni hadi wao wamtafute. Wakiongea nae kwenye simu huwaambia wamsalimie baba yao licha ya kuwa alifariki miaka mingi iliyopita.
Nimesikia Kamanda wa Polisi Dar, SACP Mambosasa akisema kuwa polisi wamefuatilia na kugundua kuwa Dr.Shika hana makazi ya kudumu jijini Dar es Salaam. Anaishi kwenye chumba kimoja cha kupanga na anadaiwa malimbikizo ya kodi.
Kifupi, nimeguswa sana na jina la SHIKA pia sura yake kama mtu ninayemfahamu vizuri tangu tukiwa majirani kijijini wakati huo Shika na Jeremiah wakisoma darasa moja kwenye Shule ya msingi Chamugasa pamoja na dada yangu mkubwa Magdalena. Hivyo, sura hii ndiyo sura pia ya mdogo wake aliyeko kijijini Chamugasa aitwaye Pius na mdogo wao mwingine Daudi.
Ikiwa huyu ndiye Dr.Shika ninayemfahamu, daktari bingwa wa magonjwa ya akili basi nimeumizwa mno na mfumo wa maisha yake. Licha ya kwamba tunatoka kijiji kimoja lakini kama mtanzania wa kawaida sikutegemea daktari bingwa awe katika maisha haya.
Kuna watu wanaweza kumbeza Dr.Shika lakini hatujui nini kilimpata. Hatujui huko Urusi alifanyiwa nini. Hatujui huyo mwanamke aliyemuoa huko ilikuaje wakaachana. Hatujui kama walifanikiwa kupata watoto. Hatujui kwanini serikali ilishindwa kumsaidia Dr.Shika wakati ilitumia kodi za watanzania kumsomesha nje ya nchi.
Bila shaka Dr.Shika alipaswa kuwa katika nafasi ya kuisaidia jamii yake kupitia elimu yake. Ilitegemewa sasa hivi awe daktari mwandamizi mshauri, ambaye madaktari junior wanaenda kupata maelekezo kwake. Au alipaswa kuwa mhadhiri chuo kikuu cha Sayansi ya tiba kama MUHAS, CUHAS au KCMC akihamisha maarifa yake ya udaktari kwa wanafunzi wa udaktari.
Lakini yupo mjini tu anahangaika. Anaishi chumba kimoja peke yake. Hana mke, hana mtoto, hana nyumba, hana gari, hana mifugo. Yuko peke yake.
Hatimaye ameingia kwenye biashara ya utapeli. Kutoka udaktari bingwa hadi utapeli. Na afya yake inavyoonekana ni mlevi wa kupindukia hadi midomo imebabuka. Huenda anakunywa pombe kali za kienyeji kama chang'aa na mataputapu mengine. Pia inawezekana hana muda wa kula. Mtu anayeishi peke yake atapika saa ngapi? Nani atamkumbusha kula? Lazima afya yake itadorora.
Bila shaka hakupenda kuwa katika hali hiyo. Huenda yupo kwenye msongo mkubwa wa mawazo. Kwa kifupi Dr.Shika si timamu tena. Anahitaji usaidizi wa hali na mali.
Kumdhihaki na kumuacha apotee haitasaidia kitu. Zaidi sana taifa ndio litapata hasara kwa kutumia rasilimali zake kumsomesha mtu aliyegeuka mzigo kwa taifa. Mimi naamini Mwalimu Nyerere alipowasomesha Shika na kaka yake alikuwa ana matumaini makubwa nao, kwamba watasaidia taifa. Hebu fikiria Shika angekuwa timamu angesaidia watu wangapi? Leo kuna watu wanakufa kwa kukosa madaktari, lakini kuna madaktari kama Dr.Shika wapo tu mtaani hawajielewi, wameangukia kwenye ulevi wa kupindukia na utapeli.
Serikali iangalie namna ya kuwasaidia watu wa aina hii kwa maslahi ya taifa. Naamini hata madaktari waliosoma na Shika Urusi, au waliofanya nae kazi Muhimbili wana nafasi ya kumsaidia kama wataamua kufanya hivyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com