Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WABUNGE WAELEZA KUWA NA WOGA WA KUHOJI NA KUIDADISI SERIKALI

Baadhi ya wabunge wameeleza kuingiwa woga wa kuhoji na kudadisi masuala mbalimbali kutokana na kutishiwa kutopatiwa fedha za miradi ya maendeleo majimboni kwao.



Kauli hiyo waliitoa wakati wakichangia semina ya wabunge juu ya jukumu la Bunge katika kufuatilia kikamilifu matumizi ya Serikali yaliyofanyika kwa kamati saba za Bunge.


Kamati hizo ni Kamati ya Bajeti, Kilimo, Mifugo na Maji, Viwanda, Biashara na Mazingira, Huduma za Jamii, Utawala na Serikali za Mitaa na Hesabu za Serikali za Mitaa.


Akizungumza katika semina hiyo, Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema wabunge wamekuwa waoga kusemea tofauti na Bunge la 10 na kwamba hoja zinajengwa kisiasa na wengine wanapohoji wanaambiwa hawatapelekewa fedha majimboni.


Alisema jambo linalowafanya wabunge kutosema yale wanayoyataka wananchi ni siasa kuingia bungeni tofauti na mabunge yaliyotangulia ambapo wabunge walikuwa wakiacha siasa lango kuu la kuingilia bungeni.


“Jambo hili linaweza kuwa linasababishwa na viongozi wa bunge ama serikali ambapo hoja zenye manufaa zinaweza kupelekwa bungeni, lakini wakaamua kuziua,”alisema Selasini.


Kwa upande wake, Mbunge wa Mpendae (CCM) Salim Hassan Turky, alisema mambo yote waliyoelezwa wanayajua, lakini kuna kitu kinachomoza bungeni na kinaondoa uhai wa bunge.


“Hasa unapohoji na kudadisi basi na wewe unaitwa na kuhojiwa na kudadisiwa," alisema Turky, "kwa hiyo wabunge wote wanakuwa waoga wa kuuliza maswali".


"Sasa sijui kama utaratibu huu utafanya haki itendeke?”


Aliomba viongozi wa Bunge wakaliangalie hilo na kwamba endapo wakisimamia serikali vizuri wataweza kutekeleza majukumu yao.


Naye Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara alisema kuwa tatizo lililopo ni Bunge kutofanya kazi inavyotakiwa.


“Inafikia Bunge mtu akisema hapana, waliosema hapana wasipewe fedha za maendeleo kwenye majimbo yao wakati hayo mambo hayakuwapo,” alisema Mbunge huyo.


Alisema wabunge sasa wanaogopa kuisema au kuikosoa serikali licha ya kuwa Bunge limeundwa ili kusema kero za wananchi.


“Bunge limebaki kuwa la muhuri na sio Bunge, na sisi hapa tunakuja kwa ajili ya posho na mishahara tu tuliyoambiwa,” alisema Mbunge huyo.


Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM) alisema nguvu ya Bunge ya kuisimamia serikali ni ndogo kutokana na ukosefu wa fedha.


“Ili tuweze kuwa na mchango madhubuti lazima tujengewe uwezo wa kushughulikia taarifa mbalimbali, Bunge lihakikishe linatujengea uwezo kwenye nyanja mbalimbali wabunge ili kuisimamia serikali ipasavyo kwenye masuala mbalimbali ikiwamo bajeti,” alisema.


Mbunge wa Ileje (CCM), Janet Mbene ambaye alikuwa mwenyekiti wa semina hiyo, alisema kwa umoja wao wabunge wakisimama kwa pamoja serikali itawasikiliza na hawatafanya kazi kwa woga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com